The House of Favourite Newspapers

Msukule aliyekutwa kwa tajiri mengi yafichuka

2

IMG_1471Mume wa Upa akiwa na watoto wao.

Stori: Makongoro Oging’, UWAZI
DAR ES SALAAM: Yule mwanamke ambaye gazeti hili lilitoa habari zake wiki iliyopita yenye kichwa; MASWALI 9 ‘MSUKULE’ KUKUTWA NYUMBA YA TAJIRI na baadaye kutoweka Kituo cha Polisi, Mbezi, amepatikana katika Bonde la Mto Msimbazi, Tabata jijini Dar wiki iliyopita na sasa yupo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi.

Kufuatia maswali mengi kuhusu mwanamke huyo kukutwa ndani ya shimo la maji machafu ambalo halijaanza kutumika nyumbani kwa mfanyabiashara Mtei, Kibamba, Dar, Januari 19, 2016 na watu kudhani ni msukule, sasa majibu yamepatikana kwa sehemu kubwa.

KAWAIDA YA GAZETI LA UWAZI
Gazeti la Uwazi kama ilivyo kawaida yake, lilifanya kazi ya ziada ili kuhakikisha ‘ei tu zedi’ ya mwanamke huyo inapatikana na wasomaji wanaijua kwani tukio lake liliibua sintofahamu kubwa miongoni kwa jamii.Uwazi liliwatafuta ndugu wa karibu wa mwanamke huyo na kuzungumza nao kwa kirefu.IMG_1478

JINA LAKE NA UMRI
Awali jina kamili la mwanamke halikupatikana lakini sasa imebainika anaitwa Mariam Salehe Jumanne lakini ni maarufu kwa jina la Upa. Alizaliwa mwaka 1986 kwenye Kijiji cha Masaki, Kisarawe, Pwani. Kwa hiyo kwa sasa ana umri wa miaka 30. Awali gazeti hili lilimkadiria kuwa na miaka 27 kutokana na mwonekano wake katika picha.

DADA YAKE AANIKA UKWELI
Uwazi lilifanikiwa kukutana na dada wa Upa aitwaye Mwasiti Tarimo. Alikuwa na haya:
“Upa ni mtoto wa pili kati ya watano kwa baba na mama yetu. Tulikuwa naye hapa kwangu (Tabata Matumbi, Dar) tangu Januari 2, mwaka huu akitokea kwa mume wake Masaki, Wilaya ya Kisarawe. Alikuja kunisalimia na alifuatana na watoto wake wawili, Jumanne Issa (3) na Mohamed Issa (miezi 9).

“Akiwa hapa, baada ya siku mbili aliniaga kuwa anakwenda Buguruni Sokoni kuwanunulia nguo watoto wake lakini hakurudi.

GPL_4562 48Mama mzazi wa Upa akiongea kwa masikitiko.

ALIPOONDOKA NYUMBANI
“Alipoondoka alivaa suruali na tisheti nyeusi. Baada ya siku 2, tukatoa taarifa kwa ndugu wa Buguruni baada ya kuona harudi. Wao walisema alifika hapo kwao lakini akaondoka akidai anakwenda Vingunguti kwa ndugu mwingine. Tulipofuatilia huko walisema alifika na kuondoka. Sasa hatukujua alipo.”

PICHA MTANDAONI
Dada anaendelea: “Baada ya kuona hakuna matumaini ya Upa kurudi na zimepita siku kadhaa, siku hiyo tukiwa tunajiandaa kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Tabata tukaona picha zake mtandaoni akiwa mtupu huku akitolewa shimoni nyumbani kwa Mtei. Tulichanganyikiwa sana, mama yetu ambaye nipo naye hapa alizimia kwa muda mrefu ikabidi tumkimbize Zahanati ya Tabata.

WAENDA POLISI MBEZI
“Baada ya hapo tulikwenda Kituo cha Polisi Mbezi ambapo walikiri kumtoa katika shimo lakini aliwatoroka baada ya kumuogesha wakijiandaa kumpeleka Hospitali ya Tumbi (Kibaha, Pwani) kwa uchunguzi.

WAENDA MOCHWARI MUHIMBILI
“Ilibidi twende Tumbi ambapo walituambia hayupo mwanamke kama huyo. Tukarudi Polisi Mbezi lakini nao hawakumuona. Wakasema tuache namba ya simu ili akipatikana tutaarifiwe, tulifanya hivyo kisha tulikwenda Muhimbili kwenye chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari) lakini pia hatukumpata. Tuliamua kurudi nyumbani.

IMG_1480….Ndugu zake.

JANUARI 23, 2016
“Ilipofika Januari 23, tulipata taarifa kuwa Upa amepatikana Bonde la Mto Msimbazi na amechukuliwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Buguruni. Tulipokwenda tulimkuta, tukamchukua na kumuogesha tena kisha tukafuatana na polisi hadi Muhimbili kufanyiwa uchunguzi. Upa aliwahi kupata ugonjwa wa kifafa cha uzazi alipojifungua mtoto wa kwanza.”

HISTORIA YA UPA KWA UFUPI
Fatuma Pembe ni mama mzazi wa Upa. Alionekana mnyonge kupita kiasi kwani hakuamini kama mwanaye angekutwa na kadhia hiyo. Hapa anazungumzia historia ya mwanae kwa ufupi:

“Upa alipomaliza Shule ya Msingi Masaki alikaa kidogo, mwaka 2008 akapata mume wakafunga ndoa mpaka Mungu akawajalia kupata watoto wawili. Kwa sasa naomba uniache sijapata nguvu, siwezi kuongea.”

MUME WA UPA SASA
Issa Mohamed ni mume wa Upa, yupo jijini Dar tangu apate taarifa ya kutoweka kwa mkewe. Alipohojiwa wiki iliyopita akiwa Buguruni Malapa kwa shangazi yake, Maua Salehe. Alikuwa na haya ya kusema:

msukulee-001“Wiki tatu zilizopita nilipata taarifa kuwa mke wangu hajaonekana wala hajulikani alipo, ndiyo ikabidi nije hapa Dar ili kumtafuta. Lakini baada ya muda alipatikana na kupelekwa Muhimbili kwa uchunguzi.

WATOTO WAKE WAMLILIA
“Kwa sasa nipo na watoto wangu hapa kwa shangazi, nasubiri apate unafuu nimchukue turudi nyumbani Masaki. Nimekuwa nikimpelekea chakula hospitalini na tumekuwa tukila naye pamoja huku akiniulizia kuhusu hali ya watoto wetu. Namwambia wanakulilia sana hasa mkubwa wa miaka mitatu.

WAPIGAPICHA WALIOMPIGA PICHA UPA
“Ila nawalaani wale wote waliompiga picha mke wangu akiwa mtupu na kurusha mtandaoni. Kwa kweli hawakumtendea haki kama binadamu mwenzao. Wanaweza kufanya hivi leo kwa mke wangu lakini kesho ikawa kwao.”

UWAZI MUHIMBILI
Mwishoni mwa wiki iliyopita, gazeti hili lilifika Ofisi za Uhusiano Hospitali ya Muhimbili na kumkuta afisa mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Neema Mwangomo ambapo alikiri kumpokea Upa na kwamba yupo katika kitengo cha wagonjwa wa akili kwa uchunguzi zaidi.

2 Comments
  1. ngwachi says

    Ushauri wa bure : Kuna uponyaji wakimwili na wakiroho – Upa anahitaji uponyaji wa kiroho – mpelekeni akaombewe – nenda ubungo maji Ufufuo na uzima – si dhihaka atapona!!!

  2. alex rodrick says

    eeh inatisha!!!

Leave A Reply