Msuva Aanza Hesabu za Kusepa Yanga SC

STORI: Wilbert Molandi | CHAMPIONI JUMATATU| Dar es Salaam

WINGA machachari na tegemeo wa Yanga, Simon Msuva, amesema ana maisha mafupi ya kuendelea kuwepo katika timu hiyo huku akiendelea kuweka mipango yake ya kuondoka Jangwani. Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumalizika kati ya Yanga na Zanaco ya Zambia iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na matokeo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Nyota huyo, hadi hivi sasa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuichezea timu hiyo inayofundishwa na Mzambia, George Lwandamina. Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema ana malengo na ndoto nyingi za kucheza soka la kulipwa, hivyo hategemei kukaa muda mrefu Yanga.

Msuva alisema ni mapema kuweka wazi katika kipindi hiki ambacho bado ana mkataba na Yanga, kila kitu atakiweka wazi mara baada ya mkataba wake kumalizika. Aliongeza kuwa, ana ofa nyingi amezipata ndani na nje ya nchi ambazo kwa sasa amezifanya siri huku akiendelea na majukumu mengine ya kuipambania timu yake.

“Hivi unavyotegemea mimi nitaichezea Yanga milele? Hapana, nina mipango mingi niliyoweka mara baada ya mkataba wangu wa mwaka mmoja kumalizika. “Nisingependa kuweka wazi kila kitu changu ninachokifanya katika kipindi hiki, zipo ofa nyingi lakini huu siyo muda wake, kwani nimebakisha mwaka mmoja wa kuendelea kuichezea Yanga.

“Bado ninaendelea kuipenda timu yangu ya Yanga inayoniajiri na kunilipa mshahara mzuri, lakini ijulikane kuwa mimi sitaichezea Yanga milele,” alisema Msuva.

Loading...

Toa comment