The House of Favourite Newspapers

Msuva Ambariki Samatta Kutua Aston Villa

0

WINGA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na klabu ya Difaa El Jadid ya Morocco, Simon Msuva, amefunguka kufurahishwa kusikia taarifa za nahodha wake wa Stars, Mbwana Samatta kukaribia kujiunga na timu ya Aston Villa inayoshiriki katika ligi maarufu duniani ya England.

 

Samatta anakaribia kutua Aston Villa akitokea KRC Genk ya Ubelgiji. Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema kama Samatta akikamilisha usajili wake Aston Villa, itakuwa ni daraja kwa wachezaji wengine wa Kitanzania kufika huko.

 

“Ni jambo zuri sana kuona mchezaji mwenzetu Mtanzania anakaribia kujiunga na ligi maarufu zaidi duniani ya England, kwangu nafurahishwa kwa kuwa atatufungulia milango wachezaji wengine wa Kitanzania baada ya yeye kufika huko.

 

“Ni wajibu wetu sasa wachezaji kupambana kuhakikisha tunayafikia malengo yetu, kwani hakuna linaloshindikana kwa sasa kwenye mpira kama tukionyesha kiwango kizuri pamoja na kujituma, baada ya Samatta tunatamani kuona wachezaji wengine tukifika huko alipo yeye,” alisema mchezaji huyo.

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply