Msuva Amzima Kichuya, Yanga Yafunga Mabao 35
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam, Championi Jumatano Toleo la Januari 4, 2017
YANGA juzi ilifanikiwa kufungua mwaka kwa kishindo zaidi baada ya kuichapa timu ya Jamhuri ya Pemba kwa mabao 6-0 kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi.
Huu ulikuwa muendelezo wa Yanga wa kupachika mabao mengi kwenye michezo yake ambayo imecheza kuanzia Agosti, mwaka jana, lakini kikiwa ndiyo kichapo kikubwa zaidi wamekitoa kuanza kipindi hicho.
Mbali na Yanga, Simba nao wamekuwa wakikutana na baadhi ya timu na kuzipa dozi kubwa ambapo leo Championi linachambua ni mchezaji gani kinara wa kupachika mabao pale timu hizo zinapofunga kuanza mabao matatu na kuendelea kwenye mchezo mmoja.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva (kulia) akishangilia na wachezaji wenzake.
Katika idadi hiyo ya mabao kuanzia msimu huu ulipoanza mwezi Agosti, Yanga wanaonekana kuwa kidedea kwa kutoa dozi nene zaidi baada ya kushinda michezo tisa kwa mabao matatu au zaidi huku Simba wao wakishinda michezo minne tu kwa mabao matatu au zaidi, ambayo ni nusu ya ile ya Yanga.
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.
Katika uchambuzi huo, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva ameonekana kuteka nchi baada ya kuwa kinara wa kupachika mabao kwenye michezo hiyo huku akimwacha mbali kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya.
Yanga katika michezo hiyo tisa ambayo wameshinda kwa idadi hiyo ya mabao, Msuva amefanikiwa kufunga mabao nane, huku timu jumla ikifunga mabao 35.
Msuva ambaye kwa jumla kwenye ligi ana mabao tisa, anaonekana kuwa kwenye michezo hiyo mingi alikuwa akifunga mabao mawili-mawili.
Wakati Yanga walipoichapa JKT Ruvu mabao 3-0, yeye alifanikiwa kupachika mawili, pia mchezo wa juzi dhidi ya Jamhuri alifunga mawili.
Mabao mengine alifunga kwenye mchezo dhidi ya African Lyon waliposhinda mabao 3-0, ambapo alifunga bao moja, dhidi ya Mtibwa Sugar walishinda 3-1 yeye akafunga bao moja, Kagera Sugar walishinda mabao 6-2 ambapo alifunga bao moja, lakini pia kwenye mchezo wa pili dhidi ya JKT Ruvu alifunga bao moja.
Kikosi cha timu ya Simba.
Mchezaji wa Yanga anayemfuatia Msuva kwa kupachika mabao kwenye michezo hiyo ni Donald Ngoma, ambaye ana mabao saba akifuatiwa na Amissi Tambwe ambaye ana mabao sita, huku Obrey Chirwa akiwa na manne, Deus Kaseke ana matatu, Vincent Bossou na Juma Mahadhi wana mawili kila mmoja na Kamusoko ana moja.
Wakati Simba wenyewe wakiwa ndiyo vinara kwenye Ligi Kuu Bara huku Kichuya akiwa ameshafunga mabao tisa, kwenye michezo minne ambayo timu yake ilishinda kuanzia mabao matatu na kuendelea yeye amefanikiwa kuwa kinara kwa kupachika mabao manne tu, yakiwa ni nusu ya yale ya Msuva.
Simba ambao msimu huu wamekuwa wakishinda kwa mabao 2-0, 2-1 au 1-0 mara nyingi, walifanikiwa kupata ushindi mnono kwenye mchezo dhidi ya Majimaji ambapo walishinda kwa mabao 4-0 na Kichuya akafanikiwa kupachika mawili.
Huu ndiyo ulikuwa mchezo wao waliotoa dozi kubwa zaidi, mingine ambayo wameshinda kwa ushindi mkubwa ni dhidi ya Ndanda, Toto African na Mwadui, yote hiyo wameibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Jamal Mnyate, ambaye amefungana na Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo pamoja na Mohamed Ibrahim kila mmoja akiwa amefunga mabao mawili, hawa wanaonekana kuachwa mbali sana na mshindi wa pili wa Yanga.
Hawa wameachwa na Ngoma kwa mabao matano na ukiunganisha mabao yao yote kwa pamoja, wanafikisha nane ambayo ndiyo yanakuwa sawa na ya Msuva.
Hakika hata kama Yanga hawatatwaa makombe msimu huu lakini watakuwa wamegawa dozi za hatari kwa wapinzani na ni dhahiri wana safu kali ya ushambuliaji msimu huu.
Matokeo makubwa ya Yanga
Yanga 3-0 African Lyon
Kaseke
Msuva
Mahadhi
Yanga3-0 Majimaji
Kaseke
Tambwe
Tambwe
Yanga 3-1 Mtibwa Sugar
Chirwa
Msuva
Ngoma
Kagera Sugar 2-6 Yanga
Donald Ngoma
Simon Msuva
Obrey Chirwa
Deus Kaseke
Obrey Chirwa
Donald Ngoma
Yanga 4-0 JKT Ruvu
Obrey Chirwa
Amissi Tambwe
Simon Msuva
Amissi Tambwe
Yanga 3-0 Mbao
Bossou
Emmanuel Mseja (OG)
Tambwe
JKT Ruvu 0-3 Yanga
Michael Aidan (jifunga)
Msuva
Msuva
Yanga 4-0 Ndanda
Amissi Tambwe
Donald Ngoma*2
Vincent Bossou
Yanga 6-0 Jamhuri
Msuva *2
Ngoma *2
Mahadhi
Kamusoko
Matokeo makubwa Simba
Simba 3-1 Ndanda
Laudit Mavugo
Frederic Blagnon
Shiza Kichuya
Simba 4-0 Majimaji
Mnyate
Kichuya
Mnyate
Kichuya
Simba 3-0 Toto African
Mzamiru Yasin
Laudit Mavugo
Mzamiru Yasin
Mwadui FC 0-3 Simba
Mohammed Ibrahim
Kichuya
Mohammed Ibrahim
Comments are closed.