The House of Favourite Newspapers

Msuva apata dili TP Mazembe

0

NgassanaMsuva.jpgHans Mloli na Said Ally

MFUATILIA vipaji wa TP Mazembe, Patrick Kasangara, amechukua majina ya Simon Msuva, Haji Mwinyi na Said Ndemla na mpango alionao ni kuyafikisha kwa bosi wake Moise Katumbi ili wasajiliwe.

Kasangara alikuwepo nchini kufuatilia vitu vitatu ndipo alipokutana na Msuva na Mwinyi ambao wamemvutia na akaamua kuondoka na majina yao kwenye begi lake.

Jambo la kwanza lilikuwa kuleta magari mawili ya nyota wa TP Mazembe, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, pili ni kuangalia viwango vya wachezaji hao katika mechi ya Taifa Stars na Malawi na mwisho ni kutazama nyota wa Stars wanaoweza kujiunga na TP Mazembe.

Kasangara aliliambia Championi Jumamosi kuwa, Ndemla wa Simba anamfuatilia kwa muda mrefu na sasa amejiridhisha na uwezo wake, lakini akajikuta pia anavutiwa na Msuva na beki wa kushoto Haji Mwinyi, wote wa Yanga.

“Msuva na Mwinyi watasajiliwa TP Mazembe lakini tutawapeleka SC Don Bosco kuwakuza kisha tuwatumie baadaye, nimeridhika nao kwa kweli, ila Ndemla anaweza kwenda TP Mazembe moja kwa moja,” alisema Kasangara.

Don Bosco ni timu inayomilikiwa na Champion Katumbi ambaye ni mtoto wa mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi. Mazembe na Don Bosco zote zinashiriki Ligi Kuu DR Congo katika Jimbo la Lubumbashi na mikoa ya karibu yake.

“Hivi ndivyo tunavyofanya mara kwa mara tunapotaka kupata wachezaji wapya chipukizi, nafanyia kazi usajili huu,” alisema Kasangara.

Hivi karibuni TP Mazembe ilionyesha nia yake ya kumsajili Ndemla lakini ikawa kimya hadi sasa alipoibuka Kasangara kuendelea kujiridhisha na uwezo wake.

Don Bosco msimu ujao inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya DR Congo huku TP Mazembe ikiwa bingwa.

Timu hiyo ina uhusiano wa karibu na TP Mazembe na zote zinatokea Lubumbashi na hutumia uwanja mmoja kwa mechi zao na kuna wakati mchezaji aking’ara Don Bosco hupelekwa TP Mazembe.

Pia mchezaji anayeshuka kiwango TP Mazembe hupelekwa Don Bosco kujiweka fiti.

Leave A Reply