Mtaani kwetu kimenuka!

 

 

 

Waswahili siku hizi wana neno lao utasikia ‘kimenuka’, ukisikia hilo ujue mambo yamekaa fyongo, basi hapa mtaani kwetu habari ndiyo hiyo. Uchaguzi ndiyo huo unakuja, homa inazidi kupanda, bendera za kila rangi zinaongezeka, maspika yanaongezeka nguvu, kila upande unaelezea jinsi utakavyoboresha maisha yetu, na hicho ndicho wananchi tunachokitaka.

Ishu hapa ni kupata viongozi watakaotuletea maendeleo na kuboresha hali tuliyo nayo, na kuendeleza amani.  Na kwa kuwa wote wanaotaka kutuongoza ni wananchi wenzetu, basi hakuna ugomvi wala nini, atakayechaguliwa tunamuachia uwanja atekeleze aliyotuahidi ili mambo yetu yawe safi.

Sasa hapa kwetu kuna jamaa yetu mmoja anagombea udiwani, jamaa mmoja fresh sana, mkimya, mtaratibu hata kabla hajaanza mambo ya kugombea alikuwa anajulikana sana hapa mtaani kwa hulka zake hizo, lakini mkewe ndiye aliyejulikana zaidi, ingekuwa vipi tungemuita mmoja wa masupastaa hapa mtaani.

Ee bwana mama anaongea huyo, mama mbishi huyo, sijapata kumuona, kuna watu wanadai kuna siku aliwahi kuanza kubishana na mtangazaji kwenye TV mpaka ikalazimu mtangazaji akatishe taarifa ya habari na kuingiza tangazo, kisha kulalamika kuwa kila anachosema kuna mtu anambishia.

Mtaani ilijulikana kuwa usije ukapata bahati mbaya mkaanza kubishana, maana hatimaye utashindwa tu kwa aibu. Kipaji chake hiki angekitumia kutungia mashairi vikundi vya mipasho hakika angekuwa  na mkwanja mrefu, na kwa vyovyote vile angekuwa na umaarufu wa Kitaifa na Kimataifa, kipaji hiki pia angeweza kurekodi wimbo wa Hip Hop ungekamata chati maana pia alikuwa na spidi kali ya kuongea, kujumlisha yote hayo alikuwa na sauti ambayo ilikuwa haihitaji spika, utamsikia tu.

Sasa kisa cha watu kusema kimenuka, kumetokea mpasuko nyumbani kwa mgombea udiwani wetu, mwanzo walianza vizuri na mama akiwa kampeni meneja wa mzee, sasa bwana, si mgombea urais wa kambi moja akaja kufanya mkutano jirani na kwetu, mama akashawishika akarudisha kadi, akahama chama.

Kuanzia hapo kila mzee akiitisha mkutano, mama anakaa nyuma ya umati na kujibu kila hoja inayotolewa, kiasi kwamba watu wanaacha kumsikiliza mgombea wanamsikiliza mama wa mipasho, juzi nimemuona wazi mgombea machozi yanamlengalenga sijui kwa hasira au uchungu, maana kila anachosema mama anakipinga kwa mifano ya kinachotokea kwenye ndoa yao….yaani kimenuka!

 

Loading...

Toa comment