The House of Favourite Newspapers

MTI WA MBUYU HAUKATWI KWA SHOKA

NDIYO hivyo sema wee mpaka koo likauke na sauti isitoke kabisa elimu yangu kama maji, usipoyanywa utapikia ugali ule, hee heeeiyaaaaaa!

Utashanga sana na mwaka unakatika huu! Janamke zima, miaka karibia thelathini linagoma kuolewa, umekuwa mgomba wewe kusema utakatwa ndizi lakini hauzeeki! Haloooo ehhhhhh! Langu dera miye mchana sare usiku night dress, upo?

Shoga hata kama mume wa mtu anakujali sana tena kuna wengine wakishapata mume wa mtu utawasikia tu kwenye bomba, ‘ohh kuolewa utumwa acha niendelee kujilia’ hiyo ada ya watoto wake inaishia kwako na ulivyo hujui matumizi unachuna mpaka mwanaume anaomba pooo, shuuuutuuuuu!

Baada ya kukupa udambwidambwi shoga ni bora tukaingia kwa kileee kilichonikalisha kalio kuongea na wewe hapa! Shoga leo nataka tuongelee sisi wanawake ambao kutwa tuko bize kwenye vilongalonga vyetu, kuunguza mboga ni siye, kuchepuka ni siye, kuchelewesha kupikia watoto ni siye, aibuuuu!

Wakati mwingine nawasema wanawake wenzangu hadi roho inaniuma, tena wengine wananiuliza hivi shoga kwani wee mwanaume kulikoni kugeukana! Looo mnitue mwanakwetu niliyefunzwa unyagoni juu mpaka chini kumpeti mwanaume! Ndiyo maana nikaitwa kungwi wa makungwi, anayejiona amenizidi ajitokeze tushindane hadharani, aweke chini dera miye niweke mtandio, akiweka shumizi miye naweka gagulo heee

heeeiyaaaaa!

Litawachoma sana mwaka huu, shoga hakuna kitu nisichokipenda maishani mwangu kama kudharauliwa sisi wanawake japo sawa wakati mwingine tunajitakiaga wenyewe. Utakuta umebahatika kuolewa lakini sasa unaanza visa vya hapa na pale, wewe kutwa kushika kilongalonga chako na kuchati, mwanamke una magrupu 20 ya WhatsApp kama unataka kuanzisha maandamano, bado hujaingia huko Facebook ukienda Insta mama yaaangu ndiyo usiseme, mwanamke kila ukurasa wa udaku upo? Looooo!

Basi jitengenezee hata muda wa kufanya hayo mambo yako ya mitandaoni utakuta huna hausigeli, wewe ndiyo wa kuwapeleka wanao shule kama siyo kuwapikia na kuwafulia, hapo bado mumeo hujamfulia wala kumuandalia chakula! Mchana unashinda kwenye mitandao yote ya udaku, usiku mumeo yupo na watoto bado upo na simu yako bize, ndo tuseme umekuwa kastama kea au mhudumu wa mapokezi wewe!

Shoga kelele za bata hazimzuiii kuingia kwenye maji na ukitaka kujua gitaa lina sauti fuga kucha! Wakati mwingine mwanaume akiingia kwenye ndoa ni kama mti wa mbuyu haukatwi kwa shoka wala kutetereka, utajaribu kila njia ya kuudondosha utashindwa, utabaki unakuangalia tu.

Tena wengine wamebahatika kupata wanaume siyo waongeaji, basi wanavyowaonea kwenye vilongalonga

vyao, akirudi kazini akiulizwa kwa nini hujapika atasindikizwa na sonyo kama vile muziki wa kigodoro umezimwa katikati ya sherehe wakati huohuo anachati na madanga yake. Jamani ifike wakati tujiheshimu sisi wanawake, tuwaheshimu waume zetu, hivi vilongalonga wengine wanaviita mpanguso tujue jinsi ya kuvitumia bila kuwaudhi. Yangu kwa leo ni hayo, tukutane tena wiki ijayo, ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

Comments are closed.