Mtikila; shujaa aliyekufa akipambana

Christopher-MtikilaBAADHI ya watu walimtafsiri Mwenyekiti wa Chama cha Democrat (DP) na Mchungaji wa Kanisa la Full Salvation, Christopher Mtikila kama hazimtoshi f’lani hivi.

Lakini siku zote fikra ni utumwa wa mtu mwenyewe. Sikuwahi kuwashangaa waliomkebehi kwa jambo lolote Mtikila wakati wao hawawezi na hawataweza kuonesha ujasiri wa kiwango cha robo ya mwanasiasa huyo.

mtikilaa.jpgMtikila ninayemzungumzia ni mtu pekee aliyewahi kuishtaki serikali ya nchi hii na kuishinda. Narejea kesi ya mgombea huru aliyoifungua mahakama kuu na baadaye kuipeleka mahakama ya Afrika.

Wakati anashughulikia kesi hii ya mgombea huru mwaka 2013, niliwahi kumuuliza ugombea binafsi ulihusu nini hasa? Nilijua yeye ana chama chake.

Majibu aliyonipa: “Mimi sina tatizo, lakini siwezi kuwa kiongozi ninayetetea masilahi yangu, mimi nataka kila Mtanganyika awe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa sawa na katiba inavyotamka.”

Huyu ndiyo shujaa Mtikila aliyekufa akipambana kutetea haki za wananchi wanyonge kwa kufungua marundo ya kesi za kikatiba na kijinai dhidi ya kile alichoamini ‘haki haiombwi.’

Suala la kutafuta haki halikuwa jambo lililohitaji malipo kwa Mtikila; mwanasiasa huyu alikuwa tayari kupanda pikipiki, Bajaj au hata kutembea kwa miguu kwenda mahakamani kudai haki za wengi.

Alipofungua kesi ya kudai uhuru wa kufanya mikutano bila kuomba kibari cha polisi kama utaratibu ulivyotaka, mara kadhaa alikwenda mahakamani kwa kupanda magari ya usafiri wa umma.

Wapo waliomtafsiri vibaya, wakambatiza majina kibao ya kejeli, mpendakesi, mpuuzi, mwendawazi, mganga njaa na mambo mengimengi ya kumfedhehesha.

Kupenda kwake kesi kumelisaidia taifa katika mambo mengi mojawapo ni kupata uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara bila kuomba kibari polisi, jambo ambalo vyama vyote vya siasa vinanufaika nalo hadi ‘mganga njaa’ anaingia kaburini. MASKINI!!!

Sote ni wasafiri wa kurudi udongoni; apumzike kwa amani Mtikila ambaye kila nilipokutana naye nilijifunza jambo muhimu kiasi cha kuamini kuwa, upuuzi wake ulikuwa na faida kwa taifa kuliko werevu usio na msaada.

Mtikila hakuwa muoga, ilihitaji ujasiri na fikra pana kuzungumza naye, kumwamini na kumuelewa hasa pale alipotaja bila hofu dhambi za viongozi mbalimbali wa ngazi za juu serikalini, kimataifa na wa dini zote na kuwa tayari kukabiliana nao kwa ajili ya kulinda masilahi ya nchi.

Kabla ya kufanyika kwa Oparesheni Kimbunga iliyolenga kuwaondoa wahamiaji haramu, Mtikila alisambaza waraka akimtuhumu Rais Paul Kagame na Wanyarwanda kuwa wamevamia sehemu ya ardhi ya nchi yetu na hivyo kuitaka serikali kuchukua hatua.

Mtikila aliniambia waraka huo alimpelekea pia Rais Jakaya Kikwete. Sijui aliupokea au la lakini kilichotokea Wanyarwanda waliokuwa maeneo mbalimbali ikiwemo Ngara mkoani Kagera walirejeshwa makwao; huu ndiyo ushujaa wa Mtikila.

Mtikila amekuwa shujaa aliyepitiliza; waoga walijiuliza ujasiri wa kufanya ukosoaji mkubwa namna ile aliupata wapi; je hakuogopa kuuawa?

Majibu yake kila mara yalikuwa: “Watu waovu katika nchi yetu hawapaswi kupewa nafasi, lazima washughulikiwe na unaposhughulika nao kufa ni sehemu ya mapambano.”

Septemba 30, mwaka huu majira ya mchana Mtikila alipita ofisini kwangu kuniaga (maana sikujua kama atafariki dunia Oktoba 3) aliniambia:

“Tumieni magazeti yenu kuleta ukombozi wa nchi, mna magazeti mengi, andikeni kila gazeti kuhusu siasa, magazeti yenu yanaweza kuleta mageuzi makubwa kwenye nchi hii.”

Nadhani huu ndiyo wosia aliotuachia kama chombo cha habari kwamba tufanye kazi ya kuleta mageuzi ya kifikra, tuwe watu wa kutetea haki za wanyonge kama alivyofanya yeye. Pumzika Mtikila; tutaendelea kujenga ulipoishia!


Loading...

Toa comment