The House of Favourite Newspapers

Mtoto Achomwa kwa Mkasi wa Moto Kisa ‘Flash’

0

MTOTO wa kiume mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Bugoyi A, Mjini Shinyanga amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash Disk’ ya kuwekea Movie (Filamu) inayomilikiwa na bibi na mama yake mzazi.

 

Mashuhuda wa tukio wameiambia Malunde 1 blog kuwa mtoto huyo alifanyiwa ukatili huo Jumatano Desemba 1,2021 majira ya saa 2 usiku katika mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

 

Wameeleza kuwa siku ya tukio jioni, mtoto huyo alipewa Flash Disk na bibi yake aitwaye Adelida Leonard (50) na mama yake mzazi aitwaye Beatrice Mwombeki (28) ili aende eneo jirani kwa kijana anayeweka filamu na nyimbo za muziki akamwekee filamu kwenye ‘flash’ hiyo lakini mtoto huyo akiwa njiani alidondosha Flash hiyo na kurudi nyumbani kutoa taarifa juu ya kupotea kwa Flash Disk hiyo.

 

“Baada ya mtoto huyo kurejea nyumbani na kuwaelezea bibi na mama yake kuwa Flash imepotea, walimwambia aende akaitafute lakini hakufanikiwa kuipata na akaogopa kurudi nyumbani.

 

“Ilipofika majira ya usiku, mtoto alirejea nyumbani ndipo alipofanyiwa ukatili kwa kuchomwa na kipande cha mkasi wa kukatia maua/ fensi kilichochemshwa kwenye jiko la mkaa sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mgongoni, masikioni na mapajani na kumsababishia majeraha na maumivu makali”, wamesema mashuhuda.

 

Wameongeza kuwa licha ya kufanyiwa ukatili wa kuchomwa kwa mkasi wa moto, mtoto huyo alinyimwa chakula usiku huo wa kuamkia Desemba 2, 2021. 

 

Mtandao huu umeelezwa kuwa Desemba 2, 2021 asubuhi mama mzazi wa mtoto huyo alikwenda katika shule anayosoma mtoto na kuwaambia walimu kuwa amefika shuleni kufuatilia mtoto wake kwamba huwa anapigwa na wanafunzi wenzake.

 

Taarifa hiyo iliwashangaza walimu na walipomuita mwanafunzi huyo wakaona ana vidonda kwenye masikio wakamuuliza mama huyo kulikoni, ndipo akawajibu walimu kuwa mwanae amemwagikiwa maji ya moto.

 

“Baada ya mama huyo kusema mwanae kaungua maji ya moto, walimu wakabaki na maswali kwani mtoto alitaka kujieleza lakini akawa na uoga.

 

“Wakati huo huo mama huyo akaanza kusema ‘na flash ameipoteza atuambie ameipeleka wapi’ ..Mwalimu akamwambia ‘nenda nyumbani tutaongea na mtoto, acha namba za simu Flash ikipatikana tutakupigia’.

 

Mama huyo alipoondoka sasa ndipo walimu wakambana mtoto akaeleza ukweli wote na kuonesha majeraha aliyopata. Ndipo hatua za kuwakamata watuhumiwa zikafanyika”,amesema mtoa taarifa wetu.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo ni kumtuhumu mtoto huyo kuwa ameiba Flash na kwamba mbinu iliyotumika ni kuchemsha kipande cha mkasi wa kukatia fensi kwenye jiko la mkaa kisha kumuunguza sehemu mbalimbali za mwili wake.

 

Amesema watuhumiwa ambao ni Adelida Leonard (bibi) na Beatrice Mwombeki (mama mzazi) wamekamatwa na madhura amelazwa katika hospital ya rufaa mkoa wa Shinyanga.

Credit: Malunde | Shinyanga

Leave A Reply