The House of Favourite Newspapers

Mtoto Afariki kwa Kushambuliwa na Fisi Shinyanga

0

WAZAZI na walezi mkoani Shinyanga wametakiwa kuchukua tahadhari kwa watoto wao dhidi ya wanyama aina ya fisi ambao wamekuwa wakionekana katika maeneo mbalimbali na kusababisha madhara kwao ikiwemo ya vifo.

 

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba Juni 2, 2020,  wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na tukio la kushambuliwa hadi kufariki dunia kwa mtoto wa miaka miwili na nusu aliyehamika kwa jina la Charles Christian katika kitongoji cha Mwagala kata ya Ibadakuli.

 

Amesema tukio hilo limetokea Juni Mosi mwaka huu majira ya saa moja usiku wakati mtoto huyo akiwa anacheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao ambapo alijeruhiwa kwa kung’atwa na fisi sehemu za usoni na kisha kuburuzwa umbali wa mita 50 ambapo  alimuachia baada ya wananchi kumfukuza  na akakimbia.

 

“Wanyama hawa wamekuwa wakizurura ovyo hivyo ni budi kila mzazi au mlezi kuhakikisha watoto wao wanakuwa salama  kwani matukio ya watu kushambuliwa na fisi  yamekuwa ni mengi hivyo chukueni tahadhari,” alisema Magiligimba akiongea na wananchi wa sehemu hiyo.

 

Amefafanua kuwa Charles alifariki dunia akiwa njiani  kwenda katika hospitali ya rufaa ya kanda ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kukabidhiwa ndugu zake.

STORI NA SALVATORY NTANDU

Leave A Reply