The House of Favourite Newspapers

 Mtoto Ajinyonga Akisonga Ugali

MTOTO aliyejulikana kwa jina la Maria Saidi Mtengwa (16) mkazi wa Salasala jijini Dar amekatisha uhai wake kwa kujinyonga kikatili wakati akiandaa chakula cha mchana huku chanzo kikiwa hakijulikani.

 

Tukio hilo lilitokea Agosti 6 mwaka huu ambapo mtoto huyo alijinyonga kwa kutumia mtandio muda mfupi baada ya kukoroga uji kwa ajili ya kusonga ugali wa chakula cha mchana.

 

Akizungumza na Uwazi, jirani wa marehemu aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa familia alisema: “Siku hiyo marehemu aliamka vizuri tu, wakati akifanya shughuli zake nje, mjomba wake alitoka akielekea kazini na marehemu akamtania kwa kumwambia; ‘mbona unaenda kazini ukiwa mchafu wakati Makonda amesema ukienda mjini uwe msafi’. Akamwambia atoe nguo zake ili amfulie.

“Kwa utani ule mjomba wake akarudi ndani huku akicheka, akatoa nguo zake kisha akaondoka kwenda kazini. Pale nyumbani alikuwepo mke wa mjomba wa marehemu ambaye walikuwa wakisaidiana kufua na kuosha vyombo.

 

“Baada ya marehemu kumaliza kuosha vyombo, akaingia ndani ili aanze kupika, akabandika sufuria ya uji wa ugali. Lakini ghafla akatoweka akiacha uji ukichemka, hatukujua alikuwa amekwenda wapi lakini baada ya kutafuta sana tukamkuta amejinyonga bafuni. “Mjumbe akaitwa, akawapigia simu polisi, wakafika na kuuchukua mwili kisha kuupeleka Hospitali ya Mwananyamala,” alisema jirani huyo.

 

Akizungumza na Uwazi, mama mzazi wa marehemu, Rehema Manya alisema alipigiwa simu na mtoto wa kaka yake ambaye anaishi na marehemu akimwambia aje kwa kuwa mwanaye ni mgonjwa. “Nilipigiwa simu na mtoto wa kaka yangu ambaye anaishi na marehemu. Mwanangu alikuwa akiishi kwa mjomba yake, mimi ninaishi Manzese. Akaniambia Maria amezidiwa.

 

“Ikabidi nitoke nikapande gari, lakini baada ya kunificha sana hata kabla ya kufika hospitalini wakaniambia mwanangu amefariki, kwa kweli kuanzia hapo sikuwa na kumbukumbu. Sielewi mpaka sasa kwa nini mwanangu ameamua kujinyonga, hakuwa na shida yeyote, hakuwa na ugomvi na mtu yoyote, zaidi alikuwa akisumbuliwa na mapepo ambayo tulikuwa tukimpeleka kanisani kwenye maombi.”

Naye mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Majengo Kata ya Goba, Zabron Manyama alisema: “Nilifuatwa nyumbani na mtoto wa hapo kwa akina Maria na kunipa taarifa hizo, ikabidi niende na kukuta kweli amejinyonga, nikawapigia simu polisi wa Goba wakaja na kuchukua mwili kisha kuupeleka Hospitali ya Mwananyamala.

 

“Marehemu alikuwa akisumbuliwa na mapepo ya muda mrefu. Mimi pamoja na familia yake tumekuwa tukimpeleka kanisani kwa ajili ya maombi lakini tunashangaa amechukua uamuzi huo na hajaacha ujumbe wowote ule,” alisema mjumbe huyo.

 

Kamanda wa Polisi Kinondoni, ACP Mussa Taibu hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia kifo cha binti huyo ambaye alisafirishwa juzi kuelekea Maseyu mkoani Morogoro kwa mazishi. Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huo.

Comments are closed.