The House of Favourite Newspapers

MTOTO ATUPA TUHUMA NZITO KWA POLISI

KITENDO cha kinyama alichofanyiwa mtoto wa miaka 8 (jina linafichwa) mkazi wa Vijimbweni, Kig­amboni jijini Dar kimemfanya atupie tuhuma nzito kwa jeshi la polisi nchini, Uwazi lina habari kamili.  

 

Tuhuma hizo zinatokana na madai ya mtoto huyo kulawitiwa na kuharibiwa vibaya sehemu zake za siri na kijana ali­yemtaja kwa jina moja la Pasco ambaye polisi wanadaiwa kumkatama na kisha kumwachia.

Awali chanzo chetu kililieleza UWAZI kuwa eneo la Kingamboni kuna mtoto yuko katika mateso mazito baada ya ku­fanyiwa mchezo mchafu, taarifa ambazo zilimlazimu mwandishi wetu kufika huko kwa ajili ya mahojiano. Katika hali ya kusikitisha mwandishi alipofika nyumbani anakoishi mtoto huyo alimkuta akiwa na shangazi yake akiwa amelala na kwamba habari ziliele­za kwamba hawezi kukaa kutokana na kuharibika sehemu nyeti.

 

MWANDISHI: (Anamtaja jina mtoto, kisha anamuuliza) “Mbona umelala hapa.”

MTOTO: Naumwa.

MWANDISHI: Unaumwa nini? Mtoto anaonesha hali ya kuwa na aibu am­bapo mwandishi analazimika kumu­weka sawa kisaikolojia ili angalau apate picha ya nini kilichomkuta mtoto huyo.

Aidha, baada ya kumtoa nje shangazi wa mtoto huyo ili kumuondolea hofu, ndipo mazungumzo yalianza kama ifuatavyo:

MWANDISHI: Mtoto mzuri uliumiaje huko kwenye makalio.

 

MTOTO: Pasco ameniumiza.

Hata hivyo, safari ya mazungumzo hayo ilijaa dodoso nyingi ambazo zilizidi kuweka wazi tuhuma kwamba kijana aliyetajwa kwa jina moja la Pasco amekuwa na tabia ya kumfanyia uchafu mtoto huyo mara kadhaa.

MWANDISHI: Shangazi alikupeleka hospitali?

MTOTO: Ndiyo, alinipeleka na polisi.

MWANDISHI: Polisi ulikwenda ku­fanya nini?

MTOTO: Kumkamata aliyeniumiza.

 

MWANDISHI: aliyekuumiza ame­kamatwa?

MTOTO: Shangazi kasema hatuna hela.

Kukosa fedha alikosema mtoto huyo bila kufafanua ni kwa ajili ya kazi gani ili mtuhumiwa akamatwe kulimfanya mwandishi wetu kumrudia shangazi wa mtoto huyo ili kupata undani zaidi wa tukio.

 

HUYU HAPA SHANGAZI

Akizungumza na UWAZI shangazi wa mtoto huyo,Rose Saimoni alisema kuwa alikuwa kwenye shughuli zake, aliporudi usiku ndipo alipobaini kuwa mtoto huyo alikuwa amefanyiwa kitendo hicho cha kinyama.

“Ilikuwa Septemba 16 mwaka huu ndiyo siku ya tukio lenyewe, nilirudi kama saa tano kwa kuwa huwa nauza supu maeneo ya Majengo. “Huyu mtoto mimi nimetelekezewa na mdogo wangu wa kiume anaitwa Yohana Saimoni tangu mwezi wa saba, aliniambia anatafuta chumba atakuja kumchukua lakini mpaka leo sijamuona. “Niliporudi, mtoto wangu (aliyemzaa) akanimbia mtoto (wa kaka yake) leo amerudi saa mbili na hakujua alikuwa wapi usiku huo akasema amemchapa na akaniambia huwa alikuwa kwa Pasco.

“Nilipodadisi nikagundua kuwa mtaliyompa mwanangu yalionesha kwamba huwa anaenda mara kwa mara huko kwa Pasco ambaye ni muuza duka eneo la jirani na kwamba huwa nampa fedha shilingi 200 na chakula. Rose aliendelea kueleza kuwa baada ya kumchunguza kwa kina mtoto huyo aligundua kuwa hakuwa katika hali yake ya kawaida na kwamba aliamua kumpeleka hospita­lini patakapokucha.

“Asubuhi ilipofika nikamuuliza vizuri mtoto akaniambia huwa Pasco anamwambia aingie chumbani kwake huko akiingia anamwambia avue nguo na kisha kumwingilia huku akiwa amemziba mdomo kwa shati ili asipige kelele. “Baada ya hapo nikamchukua mtoto mpaka Kituo cha Polisi cha Kigamboni, pale niliambiwa niende Hospitali, nikaenda baada ya hapo majibu yaliyotoka kwa daktari kuwa ni kweli mtoto anaingiliwa, niliumia sana.

“Nikarudi Polisi na yale majibu wakamchukua maelezo mtoto na ku­niambia kuwa nirudi nyumbani kwa kuwa usafiri wa kwenda kumchukua mtuhumiwa haupo na kwamba nirudi terehe 18, wakanipa jalada la kesi yangu KGD/RB/8226/ 2018- KULA­WITI. “Tarehe hiyo ilipofika nikaenda polisi; kwa mara nyingine askari waliokuwepo hapo wakasema usafiri hawana, wakasema kama nina hela ya mafuta niwape, nikasema mimi hela sina kwa sababu hata ndugu zangu nilipowapigia simu hakuna aliyenisaidia kutokana na hali kuwa ngumu.

Rose anasema mfuko ulipokosa fedha ya mafuta ambayo polisi wa­naotuhumiwa kuiona hawakuieleza watu alilazimika kurudi nyumbani. Anaeleza shangazi wa mtoto huyo kwamba pamoja na hali ngumu aliyo­nayo alilazimika kukopakopa fedha kwa jirani ili angalau apate fedha za mafuta ya kwenda kumkamata mtuhumiwa. “Nikarudi siku iliyofuata, wale askari polisi waliponiona wakaniuliza umepata hela ya mafuta? Nikawaam­bia nimepata elfu kumi, wakasema nisubiri.”

Rose anaeleza kwamba baada ya kuwawezesha polisi hao wapatao watatu wa kike wawili na wakiume mmoja aliondoka kwenda kwa mtuhumiwa kwa maelekezo ya mtoto ambaye amekuwa akifanyiwa uka­tili na kwamba walifanikiwa kumtia mbaroni Pasco. “Tulipomfikisha polisi kituoni, mimi nikaambiwa niondoke na kwamba polisi watanipigia simu.

“Nilikaa bila kupigiwa simu hadi tarehe 24 (Septemba) nilipowatafuta wakasema ndiyo wanakuja twende nao eneo la tukio kwa ajili ya ku­fanya upelelezi, na kweli tukakutana tukaenda kule kwa Pasco. “Kwa kuwa Pasco alikamatiwa kazini kwake ikabidi mtoto atuongoze mimi na askari nyumbani alikokuwa anafanyiwa mchezo huo, lakini kabla hatujaingia ndani askari wakamuuliza mtoto atuambie humo ndani kuna nini na nini?

“Mtoto akasema ndani kuna neti ya bluu, godoro liko chini na madumu.” Polisi wakawaita wapangaji wen­ziye na huyo Pasco, wakasema kweli ni chumba chake. “Lakini alivyopata matatizo al­imwagiza mdogo wake aje aangalie chumba na kuuza duka la bosi wake.

“Polisi wakamuita mdogo wa Pasco na kumwamuru afungue chumba cha kaka yake, alipofungua tukakuta vitu alivyotaja mtoto viko sawa na mael­ezo yake.” Shangazi alieleza. Hata hivyo baada ya polisi kufanya uchunguzi huo inaelezwa kwamba walibaini kuwa mtuhumiwa Pasco alipofika kituoni alipotosha baadhi ya taarifa likiwemo jina lake na kwamba jina aliloandikisha kituoni ni Philibert.

Rose alieleza kwamba mara baada ya mambo yote hayo kufanyan­yika aliambiwa arudi nyumbani na kwamba angepigiwa simu kujulishwa kinachoendelea. Hata hivyo, kwa mshangao alikaa hadi Oktoba Mosi bila kupigiwa simu huku taarifa zikieleza kuwa mtuhu­miwa wake aliachiwa na polisi na kwamba yuko mtaani anadunda.

“Ikabidi tarehe 2 mwezi huu ninde pale kituoni kuwauliza polisi mbona kimya sipigiwi simu? Wakaniambia kwamba faili limepelekwa kwa mwa­nasheria watanipigia tu simu, nika­omba ile PF3 (fomu ya polisi kwa ajili ya matibabu) niliyojaziwa nilipompe­leka mtoto hospitali wakanipa nikatoa nakala halisi wakabaki nayo. “Lakini cha kushangaza askari mmoja alinipiga simu tarehe 14 mwe­zi huu kuniambia nipeleke nakala ya PF3 niliyotoa kopi kwa maelezo kuwa waliyokuwa nayo wao imepotea.

“Sasa nikajiuliza imepoteaje na wal­isema faili liko kwa mwanasheria, ina maana yeye ndiyo kapoteza? Nikaona hapa tayari naanza kufanyiwa mch­ezo wa kuzungushwa ili haki ya mtoto isipatikane. “Ikabidi niende ofisi za ustawi wa jamii Kigamboni ambao ndiyo wamenisaidia sana baada ya kubaini kuwa mtoto kalawitiwa kwa mujibu wa maelezo ya daktari.

KWA NINI MTOTO ALIFANYA SIRI

Mwandishi wetu alipojaribu kumu­uliza mtoto huyo kwa nini hakusema toka mwanzo alipokuwa anafanyiwa mchezo huo alisema: “Nilipokuwa naenda kucheza anaiita ananiambia njoo nikutume, kuna wakati alikuwa ananituma nyama buchani halafu ananiambia niingie ndani kwake. “Nikiingia ananiambia nivue nguo,” alisema mtoto huyo huku akifafanua kuwa mtuhumiwa alikuwa akitumia mafuta (hakuyataja aina) ili kufaniki­sha unyama wake wa kumwingilia.

Kuhusu kusema kwa walezi wake mtoto huyo alieleza kuwa alikuwa anaogopa kwa sababu mtuhumiwa alimwambia kuwa akimwambia mtu atamuua na kwamba kila alipomaliza kumfanyia ukatilia alikuwa akimpatia kiasi cha shilingi mia mbili. Kufuatia sakata hili UWAZI lililaz­imika kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula lakini kama kawaida yake hakuweza kupatikana na hivyo kukosa upande wa pili wa habari hii ya kusikitisha.

Hata hivyo, shangazi wa mtoto huyo amewaomba viongozi wa juu wa polisi hususan IGP Simon Sirro kuliangalia tatizo hilo zito na ame­waomba wasamaria wema wasi­mame nyuma yake ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana. Aidha, shangazi huyo amewaomba wenye kuweza kumchangia fedha za matibabu ya mtoto huyo wa­fanye hivyo kutokana na hali yake ya kifedha kuwa mbaya jambo analohisi linaweza kuchangia mtoto huyo kupata madhara makubwa zaidi ya kiafya kuliko aliyonayo.

Comments are closed.

//nukeluck.net/4/5890426