The House of Favourite Newspapers

MTOTO AUAWA! MACHO, UBONGO, NGOZI VYANYOFOLEWA

LINDI: Unyama usioelezeka! Ndivyo unavyoweza kutokwa na maneno hayo baada ya kuambiwa mtoto Mutifati Abdilahi (5), Mkazi wa Kata ya Mpilipili, Manispaa ya Lindi, kudaiwa kuuawa kisha wauaji kuondoka na macho, ubongo na ngozi waliyoichuna.

 

Tukio hilo la kusikitisha ambalo limeacha simanzi kubwa kwa ndugu, jamaa na majirani, simulizi yake ilianza kwa kutoweka Mutifati Jumanne ya Aprili 9, mwaka huu majira ya saa 1:00 usiku ambapo mwili wake ulikuja kuonekana Jumapili ya Aprili 14 saa 8:00 mchana, ukiwa umelazwa juu ya tuta la mchanga eneo lenye mikoko pembezoni mwa Bahari ya Hindi.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda, walieleza mwili wa Mutifati uligunduliwa na watoto waliokuwa wakivua samaki katika eneo hilo na kutoa taarifa kwa watu wengine kuwa wameuona mdoli kutokana na mazingira ulivyokuwa.

Akizungumza na UWAZI, babu wa marehemu Mutifati, John Emmanuel Pilila alisema kuwa, mjukuu wake alipotea maeneo ya jirani na wanapoishi.

“Mjukuu wangu (Mutifati) alikuwa nyumba ya tatu kutoka hapa kwetu akicheza na mwenzake Latifah, ilipofika saa 1:00 usiku mwenzake aliitwa kuogeshwa hivyo kumuacha na yeye akirejea nyumbani kuogeshwa.

 

“Hatukujua njiani alikumbana na nini lakini baada ya kuona kimya hatumuoni, tulianza kumtafuta maeneo mbalimbali kwa ndugu na jamaa bila ya mafanikio. Tukatoa taarifa kwa uongozi wa Serikali za Mtaa wa Mpilipili, misikitini, ofisi ya kata, Kituo cha Polisi Lindi Mjini na kwenye vyombo vya babari,” alisema Pilila.

Baada ya kutoa taarifa kila kona, Aprili 14, mwaka huu wakapata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa, Said Ndambalilo juu ya kuonekana mwili wa Mutifati maeneo ya fukwe za Bahari ya Hindi.

 

“Saa 8:00 mchana tukiwa tunapata chakula, nikapigiwa simu na mwenyekiti wetu wa mtaa kuwa kuna mwili wa mtoto umeonekana. Tulipofika eneo uliopo mwili wa mjukuu wangu, tuliukuta ukiwa umelazwa juu ya tuta la mchanga kifudifudi na gauni alilovaa siku aliyotoweka likiwa limemfunika mgongoni hadi kichwani. Tukatoa taarifa polisi ambao walifika wakiwa na mtaalamu kutoka Kituo cha Afya Lindi mjini kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi,” aliongeza Pilila.

 

Edita Simon Mlaponi (50) ambaye ni bibi wa mtoto (pichani) aliyekuwa anaishi naye marehemu Mutifati aliiambia UWAZI kuwa, hakuweza kushuhudia mwili wa mjukuu wake kutokana na mazingira aliokutwa nayo lakini mmoja wa watu waliohusika kuufikisha mwili nyumbani hapo alimwambia kuwa umepasuliwa kichwa mara mbili na kuondolewa vitu vyote vilivyokuwepo ndani yake, ukiwemo ubongo na macho.

 

“Aliniambia kuwa ngozi ya mjukuu wangu ilichunwa na kupelekwa kusikojulikana,” alisema bibi Edita.

Hata hivyo, Mganga kutoka Kituo cha Afya Lindi Mjini, Dk Richard Juma akizungumzia uchunguzi alioufanya alidai kifo chake kimechangiwa na kuziba mfumo wa kupitisha hali ya hewa, kutokana na tendo la kuzama kwenye maji.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Pudensiana Protas amethibitisha kutokea kwa kifo hicho.

 

“Tulipata taarifa ya kutoweka kwa mtoto na hatimaye kupatikana akiwa amepoteza maisha na kugunduliwa na watoto watatu waliodai walikuwa wakivua samaki kando ya bahari hiyo. Tunaendelea na uchunguzi,” alisema kamanda huyo.

Marehemu Mutifati enzi ya uhai wake alikuwa akisoma Chekechekea Kanisa la Assemble of God Tanzania (AGT), karibu na Ofisi ya (CCM) Mkoa. Alikuwa anaishi na babu na bibi yake aitwaye John Emmanuel Pilila (44) na Edita Simon Mlaponi (50).

Comments are closed.