The House of Favourite Newspapers

Mtoto Kanifanya Niwe Irene Mwingine Kabisa

 

MAMBO vipi mpenzi msomaji wa safu ya Staa na Familia. Kama ilivyo kawaida ndani ya safu hii unapata kujua maisha ya ndani kabisa kati ya staa na mtoto au watoto wake, kwa maana ni makala inayoelezea maisha ya staa akiwa na familia yake mwenyewe.

 

Leo nimezungumza na muigizaji wa filamu za Kibongo, Irene Paul na kufahamu maisha halisi ya kwake na mtoto wake wa kike anayeitwa Wendo. Fuatilia hapa chiniā€¦

 

Ijumaa Wikienda: Ni nini kimebadilika katika maisha yako baada ya kumpata mtoto wako wa kwanza?

Irene: Kuna vitu vingi sana, yaani sijui nisemeje lakini kifupi maisha yangu yote yamebadilika kwani kuwa mama ni kitu kingine tofauti na usichana.

 

Ijumaa Wikienda: Najua bado unafanya mambo ya filamu sasa kama unataka kutoka mtoto huwa unamuacha na nani?

Irene: Kwanza unavyoniona mimi toka mwanzo sikupenda mwanangu akae nyumbani na dada wa kazi, nilitaka kumuangalia mwanangu hatua kwa hatua, hata mama yangu mwenyewe alinishangaa na ndivyo hivyo nikiwa na kazi zangu anakuwepo mama yangu au ndugu yangu.

 

Ijumaa Wikienda: Wakati wa ujauzito wa mtoto huyu uliwahi kutamani kupata mtoto wa jinsia gani?

Irene: Kwa kweli sikuwahi kutamani jinsia flani, mtoto yoyote ambaye angekuja kwangu angekuwa ni mtoto kwa sababu ukweli ni kwamba mimi ndio mama yake hata ingekuaje, hivyo namshukuru Mungu kumpata Wendo.

 

Ijumaa Wikienda: Ni muda gani unatenga kuwa karibu na mwanao kwa maana ya kucheza naye, kumsomesha na mambo mengine muhimu?

Irene: Napata muda mzuri tu wa kutosha kwa mwanangu maana napenda kulea na naamini jukumu la kumfanya mwanangu afurahi ni langu.

 

Ijumaa Wikienda: Nini unajivunia kutoka kwa mtoto wako?

Irene: Vingi sana ila kikubwa ni mwanangu kufanana nami kwa kila kitu.

 

Ijumaa Wikienda: Una mpango wa kuongeza mtoto mwingine?

Irene: Ndio, nina mpango huo kwani kama unavyoona nina mmoja tu, Mungu akinibariki mwingine nitashukuru.

 

Ijumaa Wikienda: Ni mama wa aina gani kwa mtoto wako?

Irene: Ni mama anayependa mtoto afuate ninachomuelekeza na nashukuru mwanangu anajua wazi mama anachokipenda na asichokipenda.

 

Ijumaa Wikienda: Mtoto wako umemlea katika maisha ya mtoto wa staa au maisha gani?

Irene: Unajua mwisho wa siku staa ni mimi, yeye si staa hivyo napenda aishi maisha yake mwenyewe anayoyapenda, ajifunze vitu tofautitofauti, akifika umri mkubwa atachagua la kufanya mwenyewe na staili ya maisha yake mwenyewe kwani wakati huo huenda na mimi nitakuwa si staa tena. Ijumaa Wikienda: Asante sana Irene. Irene: Karibu tena.

Comments are closed.