The House of Favourite Newspapers

MTOTO MIAKA 11 ALIYEJINYONGA.. SIMULIZI YA BIBI INAUMA

DAR ES SALAAM: Tukio la kifo cha mtoto Daniel Musa (11) mkazi wa Kimara- Kona jijini Dar aliyekutwa amejinyonga chumbani kwake baada ya kutoka shule likiwa bado lipo kwenye akili za watu, simulizi aliyoitoa bibi wa mtoto huyo inauma sana!  

 

Akizungumza na Amani, bibi wa mtoto huyo, Leonora Lindi alisema tukio hilo lilitokea Jumanne ya wiki iliyopita Januari 29, mwaka huu ambapo mtoto huyo hakuacha ujumbe wowote wa kwa nini amejinyonga.

 

“Siku ya Jumanne Daniel aliamka vizuri nikamuandaa, nikampa na pesa ya shule akaenda shule na akarudi saa kumi na moja akiwa na furaha tu kama siku zote, nilikuwa jikoni napika akaja akanisalimia nikamwambia chakula kipo mezani. “Akaenda kula vizuri baada ya hapo nikamwambia akaoshe friji akanijibu vizuri tu ‘sawa’, akiwa na amani tu, sasa wakati naendelea kupika akafika mtoto wangu wa pili akamuulizia Daniel nikamuambia yupo sebuleni anaosha friji akasema anataka amtume chipsi.

 

“Basi akaingia ndani hakumkuta, akaja kuniuliza mbona hamuoni Daniel ndipo akaanza kumuita nikamwambia ajaribu kumuangalia kwenye chumba anacholala,” alisema bibi huyo. Bibi huyo aliendelea kusema kuwa baada ya mwanaye kuingia chumbani alimkuta Daniel akiwa amejining’iniza na kanga ambayo alipanda juu ya meza na kufunga kwenye dirisha.

 

“Mwanangu alikuja mbio na akaniambia Daniel kajinyonga, nikamuambia hapana usiseme hivyo, akanishika mkono tukafuatana hadi chumbani kwa mjukuu wangu huyo nikakuta kweli kajinyonga, nguvu ziliniishia nikataka kumshika lakini mwanangu akaniambia usimshike mama hiyo ni kesi.

 

“Baada ya hapo tulitoa taarifa kwa majirani ambao walienda kwa balozi kumtaarifu kisha polisi ambapo walikuja kuuchukua mwili wa marehemu na kuondoka nao, kesho yake tulienda tena polisi kwa ajili ya mahojiano nikiwa na watoto wangu wawili wote wa kiume wakawekwa ndani na mimi pia nilikaa ndani kwa saa kadhaa kwa ajili ya uchunguzi wao na baada ya muda nikaachiwa lakini mpaka sasa watoto wangu hao wapo kituoni hawajatoka,” alisema.

 

Aidha, bibi huyo alisema, kifo cha mtoto huyo kimemuacha kwenye wakati mgumu kwani alikuwa ni mtoto ambaye anamsimamia kwa kila kitu ikiwemo suala la kumnunulia mavazi ya shule. Alisema hakuwa na shida yoyote pale nyumbani licha ya kuwa hakuwa akiwaona wazazi wake mara kwa mara na hawakuwa na msaada wowote.

 

“Yani alikuwa na kila kitu, alikuwa na mashati yake ya shule mengi kama unavyoona haya hapa, alikuwa mpole kwa kweli kifo chake kimeniuma sana,” alisema bibi huyo. Kwa upande wa baba mzazi wa marehemu, Musa Lindi alielezwa kusikitishwa na kifo hicho cha mtoto wake wa pekee lakini hana la kufanya zaidi ya kumuombea Mungu amsamehe huko aliko.

 

Alipotafutwa na Amani juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro kuhusiana na tukio hilo, alisema hawezi kuzungumzia chochote kwa kuwa yupo kwenye kikao. Imeandikwa na Shamuma Awadhi na Memorise Richard.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.