The House of Favourite Newspapers

Mtoto Miaka 8 Aua Mwenzake wa Mwaka 1 kwa Panga

POLISI mkoani Morogoro inawashikilia baba na mtoto wake wa miaka minane kwa tuhuma za kumuua mtoto wa jirani yao mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba kwa kumkata mapanga kichwani.

 

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita Julai 21, 2019 saa 8 mchana katika Kijiji cha Hembeti wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambapo mwili wa mtoto huyo, Greyson Valentino,  ulikutwa umefichwa kwenye shamba la watuhumiwa ukiwa na majeraha.

 

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Julai 24, 2019, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa,  amewataja watumiwa kuwa ni Said Stephen ambaye ni baba na mwanaye wa kike (jina linahifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Mpapa wilaya ya Mvomero.

 

Kamanda huyo amesema siku ya tukio baba wa marehemu, Simon Shedrack,  akiwa kanisani alipata taarifa kuwa mtoto wake amepotea na hivyo aliamua kurudi nyumbani kuanza kumtafuta kwa kushirikiana na majirani zake.

Amesema katika harakati za kumtafuta walipita kwenye shamba la mtuhumiwa na kuukuta mwili wa mtoto wake ukiwa na majeraha kichwani.

 

Kamanda huyo amesema baada baba wa marehemu kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa ili kuhoji kwa nini mwili wa mtoto wake umekutwa kwenye shamba hilo ndipo mdogo wa mtuhumiwa (jina linahifadhiwa) alipoeleza alimuona dada yake akimuua mtoto huyo kwa kutumia panga kisha kumweka shambani.

 

Mutafungwa amesema baada ya tukio hilo wananchi walimkamata mtoto huyo aliyetajwa kuhusika na mauaji hayo na kumfikisha katika kituo cha polisi Dakawa akiwa na panga alilotumia kufanyia mauaji hayo.

Comments are closed.