The House of Favourite Newspapers

Mtoto Miaka 9 Kuhitimu Digrii ya Umeme, Kusoma Udaktari, Phd

JARIBU kukumbuka wakati ukiwa na umri wa miaka tisa ulikuwa katika kiwango gani cha elimu? Jibu rahisi kwa wengi litakuwa ni elimu ya msingi hasa madarasa yale matatu ya chini.

 

Lakini hili ni tofauti kwa mtoto kutoka Ubelgiji afahamikaye kama Laurent Simons ambaye katika umri wa miaka tisa anahitimu masomo ya uhandisi wa umeme na kutunukiwa shahada ya kwanza ya masomo hayo.

Mtoto  huyo ambaye amekuwa akisoma masomo ya uhandisi wa umeme (electrical engineering) katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Eindhoven (TUE) nchini Netherlands,  yupo mbioni kuhitimu masomo hayo.

 

Masomo hayo ni moja ya masomo magumu katika chuo hicho,  jambo ambalo hata wanafunzi wa rika la makamo wamekuwa wakikiri ugumu wa somo hilo, lakini kwa Laurent hilo halikuwa tatizo bali aliendelea kubukua kitabu na sasa anakaribia kuhitimu.

Kwa mshangao mkubwa,  wafanyakazi wa chuo hicho wamekuwa wakistaajabu na kusema,  “Kama mchezo tu Laurent yuko tayari kuhitimu digrii yake mnamo mwezi wa kumi na mbili mwaka huu.”

 

Baba yake akizungumza na shirika la habari la CNN anasema, “Kisha ana mpango wa kuanza masomo ya PhD katika uhandisi wa umeme, na kwa wakati huohuo pia anasomea digrii ya madawa.”

 

“Hii si kawaida,” alisema Mkurugenzi wa Elimu ya Shahada ya Uhandishi wa Umeme wa Chuo cha TUE, Sjoerd Hulshof, kuhusu Laurent kwamba “ni mtu wa ajabu.”


“Laurent ndiye mwanafunzi mwepesi sana kuelewa; pia nimwerevu zaidi, lakini pia ni mvulana mwenye huruma sana,” anasema Hulshof.

 

Kiwango cha nguvu ya ufahamu katika akiliyake (IQ) ni IQ 145 ambapo ni asilimia moja pekee ya watu duniani kote wana uwezo wa akili ya namna hiyo.

Laurent aliiambia CNN somo analopenda ni uhandisi wa umeme na pia anasoma kidogo mambo ya madawa.

Tayari Laurent anatafutwa na vyuo vikuu vyenye hadhi ya juu kote ulimwenguni kwenda kuendelea na masomo yake ya PhD, ingawa wazazi wake ( Lydia na Alexander Simons) hawajaweza kutoa tamko rasmi ni chuo gani wanafikiria kwa mtoto wao kwenda kufanya PhD yake.

Comments are closed.