The House of Favourite Newspapers

MTOTO WA KIGOGO KUHUSISHWA MAGARI 3 YA WIZI SIRI NZITO

DAR ES SALAAM: YAWEZEKANA kuna jambo linafichwa; lakini haijulikani kwa maslahi ya nani, maana tangu kuwepo taarifa za kukamatwa kwa mtoto wa kigogo mmoja aliyepata kuwa waziri katika serikali ya awamu ya nne (jina linahifadhiwa) aliyejulikana kwa jina la Jabir Kigoda hakuna mamlaka ya usalama iliyojitokeza na kuweka wazi jambo hilo.

Wiki moja iliyopita vyanzo vya habari kutoka ndani ya jeshi la polisi vilieleza Amani kuwa Kigoda ambaye ni mfanyabiashara alikuwa mikononi mwa polisi kwa tuhuma za kukutwa na magari matatu ya kifahari yanayodaiwa kuwa ni ya wizi.

Chanzo: Magari yamekutwa nyumbani kwake Upanga (jijini Dar es Salaam).

Amani: Ni magari ya aina gani?

Chanzo: Ni BMW X6 namba zake za usajili T 270 CFP, Toyota Fortuner (T 239 DDA) na Range Rover ambalo namba zake sizikumbuki labda hadi baadaye naweza kukupatia.

Amani: Ok, kesi hii iko wapi?

Chanzo: Kituo Kikuu cha Polisi, ukitaka picha za mtuhumiwa na namba kesi naweza kukupa.

Amani: Utakuwa umenisaidia sana, tafadhali fanya hivyo.

Aidha, dakika chache baadaye Amani lilifanikiwa kutumiwa picha na namba ya jalada la kesi na hivyo kuendelea kufanya upelelezi kujiridhisha kuwa hayo yaliyoelezwa yalikuwa kweli au la. Jumapili Agosti 5, mwaka huu Amani lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZPC), SACP Lazaro Mambosasa kwa lengo la kujiridhisha na taarifa hizo.

Amani: Habari za leo

kamanda.

Mambosasa: Salama za kwako? Mara baada ya salamu hiyo na mwandishi kumwelezea kamanda huyo ishu nzima maelezo yalipofika: “…kuna mtoto wa waziri wa zamani anaitwa Jabir Kigoda tumepata taarifa…”

Ghafla simu ya Kamanda Mambosasa ikakatika na ilipojaribiwa kupingwa kwa mara tatu mfululizo haikupokelewa jambo lililomfanya mwandishi kutamtafuta Kamanda wa Polisi Ilala, ACP Salum Hamduni ambapo alisema hana taarifa na tukio hilo.

“Labda usubiri nitafute hizo taarifa kwa maofisa wangu wanaonikusanyia habari, nikizipata, nitakupa,” alisema Kamanda Hamduni, lakini hakupiga kama alivyoahidi.

Kutokana na kukosekana kwa ukweli wa tukio hilo, Amani lilirejea kumtafuta ZPC Mambosasa kwa kumtuma mwandishi ofisi kwake Jumatatu ya Agosti 6, ili akaonane na mkuu huyo wa polisi Dar es Salaam ana kwa ana.

Hata baada ya kuketishwa na wasaidizi wa kamanda huyo kwa madai kuwa mkuu hakuwepo na kwamba angerejea mchana, mwandishi wetu alitumia zaidi ya saa 6 kupewa majibu ya pili kwamba Kamanda Mambosasa hatafika ofisini kwa sababu yuko nje ya ofisi kikazi.

Jumanne ya Agosti, 7 gazeti moja (siyo la kampuni hii) liliripoti habari hiyo ikiwa haina hata afisa yeyote wa polisi aliyekanusha wala kuthibitisha uwepo wa tukio hilo.

Wa Kwanza: Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar, SACP Camillius Wambura alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo.

Wa Pili: Mambosasa alipotafutwa na gazeti hilo alisema anao wasaidizi na kwamba waulizwe wao.

Wa Tatu: Mkuu wa Polisi Uhalifu wa Kimataifa, Joseph Solomon alipoulizwa kutokana na magari hayo kudaiwa kuibwa kutoka Afrika Kusini alisema aulizwe mkurugenzi makosa ya jinai.

Wa Nne: Mkurugenzi wa Mkosa ya Jinai, DCI Robart Boaz alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo hadi aingie kwenye mfumo ili kujua ukweli.

Wa Tano: Jabir Kigoda alipotafutwa alisema waulizwe polisi. Danadana hizi ziliibua hisia ya kuwepo kwa jambo linalofichwa ambalo haikufahamika nia yake.“Amini tukio lipo na mtuhumiwa ameachiwa kwa dhamana, kinachowafanya wakubwa washikwe na kigugumizi sijui,” kilisema chanzo ndani ya jeshi la polisi.

Amani lilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ‘Ninja’ ili azungumzie suala hili na kumaliza utata na siri ya kuwepo au kutokuwepo kwa tukio hakuweza kupatikana.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

Comments are closed.