The House of Favourite Newspapers

Mtoto Wa Miaka 5 Alipua Nyumba Yao, Afariki Dunia

UTAJISIKIAJE pale unapomwacha nyumbani mtoto wako akiwa mzima halafu ghafla unapigiwa simu na majirani na kuambiwa amefariki? Bila shaka itakuwa huzuni, taharuki na maswali kibao juu ya kifo cha mwanao;

 

Ijumaa Wikienda lina mkasa mzito uliomkuta hivi karibuni Tatu Omary mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

 

Tatu amefiwa na mwanaye, Abdulrazak Shabani ‘5’ ambaye alifariki dunia katika tukio linalodaiwa lilitokana na mtoto huyo kulipua nyumba kisha naye kutekezwa na moto.

 

Bibi wa marehemu Abdulrazak, Juto Ally aliyekuwepo siku ya tukio hilo aliliambia gazeti hili kuwa: “Nakumbuka ilikuwa Alhamisi (Januari 17, mwaka huu) saa kumi jioni, watoto walikuwa wakicheza ndani ya chumba cha mwanangu (Tatu). “Walikuwa wakicheza kwa kutoka nje na kuingia ndani, baadaye watoto wengine waliondoka akabaki mjukuu wangu peke yake humo ndani,” alisema bibi wa marehemu.

 

Kinachoelezwa na bibi huyo baada ya wenzake kumwacha mtoto huyo ndani ni kutokea kwa ajali ya moto unaotajwa kuwa ulitokana na yeye kuwasha kiberiti na kuchoma sofa. Wapi alikipata kiberiti na kwa nini asubiri wenzake watoke ndiyo awashe moto, yanabaki kuwa ni maswali tata lakini ukweli unabaki kuwa, baada ya sofa hilo kuwashwa lilizua moto mkubwa ulioteketeza nyumba nzima.

 

Licha ya bibi huyo kuwepo eneo la tukio lakini anaeleza kuwa alishindwa kumuokoa mjukuu wake kutokana na yeye kuwa nje akipika na kwamba hata alipoona moto alishindwa kumuokoa mtoto huyo kwa sababu ya ubovu wa miguu yake.

 

“Kwa hiyo baada ya kuwasha moto yeye mwenyewe akabaki humohumo ndani anauangalia,” alisema bibi huyo huku akiacha maswali ya ni vipi mtoto huyo alishindwa kujiokoa kwa kutoka nje kutokana na ukweli kwamba sofa si mlipuko unaoweza kutokea kwa ghafla na kumzingira mtu?

 

Hata hivyo ni hakika kuwa, Abdulrazak aliunguzwa vibaya na moto baada ya kujificha kwenye kabati la nguo alipokuwa akijaribu kujiokoa. Pamoja na jitihada za majirani kujaribu kuuzima moto huo nusura haikupatikana kwa mtoto wala samani za ndani kwani zote ziliteketea.

 

Kibaya zaidi mashuhuda wanasema, Kikosi Maalumu cha Polisi Kitengo cha Zima Moto kilifika eneo la tukio kwa kuchelewa na kukuta sehemu kubwa ya nyumba ikiwa imeungua.

 

MAMA WA MAREHEMU ASIMULIA Katika hali ya kusikitisha mama wa mtoto Abdulrazak siku ya tukio hakuwepo nyumbani na kwamba alimwacha mwanaye akiwa na bibi yake. “Mimi siku ya tukio sikuwepo ila nilipigiwa simu na majirani wakaniambia kuwa nyumba yetu inaungua moto. “Kabla sijafika nyumbani watu walinifuata na kunizuia kuwa sitakiwi kwenda nyumbani kuona nyumba ilivyoungua, kumbe na mwanangu alikuwa amefariki na kwamba hawakutaka nione alivyoteketea.

 

“Huyu mtoto ndiyo alikuwa kama faraja kwangu kila nikimuangalia nilikuwa naona kama nimemuona baba yake, kwa sababu baba yake alishafariki miaka mitatu iliyopita. “Lakini sikufanikiwa kabisa kumuona mwanangu mpaka siku ya Ijumaa alipoenda kuzikwa, ila naambiwa tu kwamba mtoto wangu alikuwa ameungua sana, nisingeweza kumuangalia.

 

“Naumia sana lakini mwisho wa siku namuachia Mungu,” alisema Tatu huku akibubujikwa na machozi. Mbali na tukio hilo kuondoka na uhai wa mtoto Abdulrazak bado limeiacha familia hiyo katika wakati mgumu kwani mbali na kupoteza samani mbalimbali na mavazi bado nyumba nayo imeungua vibaya.

 

“Nyumba ndiyo kama unavyoiona imeungua yote, hatuna pa kulala na uwezo wa kuiezeka haupo; tunaomba watu wema waweze kutusaidia chochote walicho nacho,” alisema bibi wa marehemu Abdulrazak. Mhariri: Kwa yeyote atakayeguswa na tukio hili anaombwa kwa chochote alicho nacho aweze kuisadia familia hii iliyopatwa na janga hili zito. Mawasiliano yao ya simu ni 0782 272 801.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.