The House of Favourite Newspapers
gunners X

 MTOTO WA MZEE WA UPAKO AFUNGUKIA AFYA YA BABA’KE

DAR ES SALAAM: Baada ya kusambaa picha katika mitandao ya kijamii ikimuonesha Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Lusekelo Anthony almaarufu Mzee wa Upako kuwa kuna uwezekano anaumwa, mwanaye wa kike, Salome Lusekelo Anthony amefunguka juu ya ishu hiyo.

 

Habari hizo za mitandaoni zilizoambatanishwa na picha moja zilikwenda mbali zaidi na kudai kuwa kiongozi huyo mwenye heshima kubwa katika kueneza Injili hatunaye.

Katika hali kama hiyo huku kukiwa na utata ndipo Gazeti la Ijumaa likaamua kutafuta ukweli juu ya afya ya Mzee wa Upako.

 

IJUMAA NYUMBANI KWA MZEE WA UPAKO

Mapema wiki hii, Ijumaa lilitinga nyumbani kwa Mzee wa Upako, Kawe-Beach jijini Dar na kupata ukweli wa ishu hiyo kutoka kwa mwanaye, Salome.

MPWA AANZA

Baada ya kufika getini kwa Mzee wa Upako, Ijumaa lilikutana na mpwa (mtoto wa dada) wa kiongozi huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mohamed ambaye alipoulizwa hali ya ‘mzee’ alisema anashangazwa na kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwani mjomba’ke huyo haumwi.

 

“Unajua tulikwenda kwenye studio moja ambayo mzee alialikwa kwenye mahojiano ya asubuhi na mimi mwenyewe ndiyo nilimpeleka, sasa akiwa pale studio alipigwa picha ikatoka vibaya.

“Picha ile ndiyo ilianza kusambaa mitandaoni na kuenezwa kuwa anaumwa, lakini siyo kweli.

 

TATIZO KUHESHIMU WITO

“Nimeumizwa na ishu hiyo kwa sababu Mzee wa Upako aliacha mambo yake na kuheshimu wito kwenye hicho kituo, lakini matokea yake wakampiga picha ambayo hadi sasa imekuwa gumzo mtandaoni kila mtu anaongea lake.

“Hata kama wewe mwandishi ungekuwa na ahadi naye ningekuruhusu ukamuone uone kama ile picha na vile alivyo kama vinashabihiana ila kwa sababu huna ahadi naye, siwezi kukuruhusu uingie ndani. Kwanza hata wewe hatukuamini usije ukafanya kama wale waliompiga picha na tutamzuia kabisa mzee asiwe anazungumza maana ile picha imeleta sitofahamu kwa familia hata ndugu zake wanajua ni kweli anaumwa.

“Jumapili alikuwepo kanisani (Ubungo-Kibangu) kama kawaida na alitoa huduma.

 

MCHUNGAJI MASHIMO AJIOMBEE MWENYEWE

“Huyo Mchungaji (Daudi Mashimo) ambaye anataka kumuombea aanze kujiombea yeye kwanza,

“Kwanza ngoja nikakuitie mwanaye Salome ili naye afunguke juu ya afya ya baba yake kama kweli anamumwa au la,” alisema kijana huyo.

 

SALOME AFUNGUKA

Mara baada ya kurudi ndani ambako Salome alikuwepo baada ya kuonana na Mzee wa Upako aliwaambia yeye yupo fiti, hafi leo wala kesho.

Salome ambaye ni mtoto wa pili katika familia ya Mzee wa Upako alisema kuwa baba yake haumwi na hana tatizo lolote la kiafya.

“Yaani naishangaa mitandao ya kijamii kwa sababu baba haumwi kitu chochote.

“Baba yangu ni mzima kabisa, ile picha ilikosewa kupigwa, labda ilipigwa na simu kisha ikasambaa ikimuonesha nywele ziko vile na afya kiasi kwamba watu wameongea vibaya mno.

 

“Wapo wengine wamesema anaumwa, wengine mlevi, siyo kweli, ungekuwa umempigia simu na akakuruhusu ungeingia ndani kumuona, yupo vizuri ila amepumzika tu.

“Kuna kituo cha habari kimoja cha YouTube kimetangaza kabisa kwamba Mzee wa Upako amefariki dunia hivyo watu wakakusanyika kwamba baba yangu amekufa, hiyo imeleta shida kwa sababu hata mimi ninapigiwa simu na ndugu na marafiki wakinipa pole ya msiba wakati si kweli au wewe umeona hapa nyumbani watu wamekusanyika kweli?

“Watu waache kusambaza taarifa za uongo, watu wanampigia hadi baba simu, ndugu zake wamekuwa na wasiwasi juu ya hilo, yaani natamani ungekuwa na appointment (ahadi) naye ili azungumze yeye mwenyewe ili watu wapate uhakika,’’ alimalizia Salome na kumaliza tetesi za mitandaoni.

 

MZEE WA UPAKO SASA

Kufuatia kuzidi kuenea kwa taarifa hizo, katikati ya wiki hii, Mzee wa Upako naye alifunguka kupitia video aliyoachia mtandaoni;

“Eti nini? Nimekufa? Mimi sijafa, wala siumwi hata mafua, niko mzima, watu wangu wote muwe na amani, eti nini!!? Nimekufaa!!. Nitabaki kuwa juu, nitabaki kileleni.”

 

Mzee wa Upako alimalizia taarifa hiyo huku akipiga kionjo cha Piere Mzee wa Liquid kuwa atabaki juu.

Hivi karibuni kulikuwa na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikisema kuwa mchungaji huyo hali yake ni mbaya kiafya, huku nyingine zikisema kuwa amefariki dunia.

Stori: NEEMA ADRIAN, IJUMAA

Comments are closed.