The House of Favourite Newspapers

Mtuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda Akamatwa Afrika Kusini

0
Fulgence Kayishema.

Fulgence Kayishema, mmoja wa washukiwa wanaosakwa sana wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994, amekamatwa katika mji wa Paarl nchini Afrika Kusini baada ya kutoroka kwa zaidi ya miaka 20.
Alizuiliwa Jumatano mchana katika operesheni ya pamoja kati ya mamlaka ya Afrika Kusini na timu ya Umoja wa Mataifa ambayo inawasaka watoro waliosalia.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia kesi bora za uhalifu wa kivita kwa Rwanda na Yugoslavia, inayojulikana kama International Residual Mechanism for Criminal Tribunals’ (IRMCT), Kayishema alikuwa mmoja wa watu waliotoroka mauaji ya kimbari waliokuwa wakitafutwa zaidi duniani.

Alishtakiwa mwaka 2001 na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na kushtakiwa kwa mauaji ya halaiki, kushiriki katika mauaji ya halaiki, kula njama ya kutekeleza mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu kwa mauaji na uhalifu mwingine.

Anadaiwa kupanga mauaji ya takriban Watutsi 2,000 – wanawake, wanaume, watoto na wazee – katika kanisa moja katika wilaya ya Kivumu, ambapo alikuwa inspekta wa polisi.

Alituhumiwa kushiriki moja kwa moja katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na kununua na kusambaza petroli ili kuchoma kanisa hilo pamoja na waliokuwa wanatafuta hifadhi humo.

“Hili liliposhindikana, Kayishema na wengine walitumia tingatinga kuangusha kanisa, kuwazika na kuwaua wakimbizi waliokuwemo ndani yake.

Kayishema na wengine kisha wakasimamia uhamishaji wa maiti kutoka katika viwanja vya kanisa hadi kwenye makaburi ya pamoja kwa takriban siku mbili zilizofuata,” taarifa ya IRMCT imesema.

Zawadi ya hadi $5m ilikuwa imetolewa na Marekani kwa kukamatwa kwake.

Mshukiwa ambaye amekuwa akitoroka tangu kufunguliwa mashtaka, anatazamiwa kufikishwa katika mahakama ya Cape Town siku ya Ijumaa, ripoti zinasema.

Takriban Watutsi 800,000 wa kabila na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa na Wahutu wenye msimamo mkali katika muda wa siku 100 mwaka 1994.

MAMA ALIA kwa UCHUNGU MWANAE KUFA kwa KUPIGWA RISASI, ALIENDA KUSHANGAA VURUGU za TANAPA na WANANCHI

Leave A Reply