The House of Favourite Newspapers

Mudathir Yahaya Mchezaji Bora Novemba

 

KIUNGO wa Singida United, Mudathir Yahaya amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Novemba, 2017 wa Ligi Kuu Bara akiwapiku Asante Kwasi wa Lipuli FC na Danny Usengimana wa Singida United.

 

Mudathir atakumbukwa kwa uwezo mkubwa aliouonyesha katika mchezo dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Namfua ambao uliisha kwa suluhu.

Kiungo huyo baada ya kushinda tuzo hiyo, atapewa zawadi ya shilingi milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi Kampuni ya Vodacom.

 

Kikao cha Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndicho kilipopitisha jina la Mudathir baada ya kupendekezwa na makocha waliopo katika viwanja mbalimbali vya ligi kuu.

Kiungo huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United mwezi uliopita na kuiwezesha kupata pointi saba katika mechi tatu ilizocheza na kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya nne.

 

Singida United ilitoka suluhu na Yanga, ikaifunga Mbeya City mabao 2-1 halafu ikaifunga Lipuli bao 1-0, ambapo Mudathir alicheza dakika zote 270 bila ya kadi yoyote.

Kutokana na uwezo wake kupanda Mudathir alirudishwa Taifa Stars na katika timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes na sasa yupo Kenya katika Kombe la Chalenji.

Mwandishi Wetu | Dar es Salaam

Comments are closed.