Mugalu Awachimba Mkwara Waarabu
MSHAMBULIAJI wa Simba, Chris Mugalu raia wa DR Congo, amefichukua kuwa wana kila sababu ya kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wao dhidi ya Al Ahly kwa kuwa wanacheza kwenye uwanja wa nyumbani licha ya ubora wa wapinzani wao.
Simba inatarajia kucheza na Al Ahly Februari 23, mwaka huu katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao unatarajia kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar.
Akizungumza na Championi Jumamosi,Mugalu alisema kuwa moja ya malengo yao katika michuano hiyo ni kuhakikisha wanapata matokeo katika mechi zao za nyumbani ili kujiwekea mazingira bora kufuzu hatua ya robo fainali msimu huu.
“Najua Al Ahly ni klabu kubwa na imekuwa na uzoefu wa kutosha katika michuano hiii, jambo bora ni kwamba tumeweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza na sasa malengo na yetu tumeyaelekeza katika mchezo wetu ujao ambao tunacheza nyumbani.“
Kitu kikubwa tunachokiangalia ni kuweza kushinda kwa sababu tutakuwa nyumbani na tunaelewa wapinzani wetu ni timu ya aina gani kutokana na ukubwa wake wa uzoefu na rekodi katika michuano hii, tunaheshimu uwezo wao na ubora wao lakini kwetu tunaangalia namna ya kuweza kupata matokeo mazuri kwao,” alisema Mugalu.
STORI: IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam