Mugalu: Tunaanza nao kwa Mkapa Tunawamalizia

MFUNGAJI wa bao pekee la mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, Mkongomani Chris Mugalu, amewaondoa hofu mashabiki wa Simba kwa kutamka kuwa wanawafahamu vizuri wapinzani wao Al Ahly ya Misri watakaocheza nao kesho Jumanne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mugalu alisema kuwa wanafahamu Al Ahly ni klabu kubwa yenye uzoefu mkubwa katika michuano hiyo lakini hiyo haiwafanyi wao wawaogope na badala yake wataingia uwanjani kupambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi.

 

 

Mugalu alisema kuwa hakuna kitakachoshindwa wao kupata ushindi katika mchezo huo kutokana na uenyeji walionao, hivyo watapambana kuhakikisha wanapata ushindi wa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana ugenini Misri.

 

 

Aliongeza kuwa kama walifanikiwa kupata ushindi wa ugenini dhidi ya AS Vita ya Kinshasa, Congo hawatashindwa kupata matokeo ya nyumbani watakapocheza dhidi ya Ahly.

 

 

“Tunafahamu Al Ahly ni klabu kubwa na imekuwa na uzoefu wa kutosha katika michuano hii, jambo bora ni kwamba tumeweza kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza na sasa malengo yetu tumeyaelekeza katika mchezo wetu ujao ambao tunacheza nyumbani.

 

 

“Kitu kikubwa tunachokiangalia ni kushinda kwa sababu tutakuwa nyumbani na tunaelewa wapinzani wetu ni timu ya aina gani kutokana na ukubwa wake wa uzoefu na rekodi katika michuano hii.

 

 

“Tunaheshimu uwezo wao na ubora wao lakini kwetu tunaangalia jinsi ya kupata matokeo mazuri na kikubwa tunataka ushindi wa nyumbani kabla ya kwenda kurudiana kwao, kwani tukipata ushindi wa hapa, ugenini wapinzani watacheza kwa presha kubwa,” alisema Mugalu aliyefunga bao la ugenini dhidi ya AS Vita na kuipa pointi tatu.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Toa comment