The House of Favourite Newspapers

Muhimbili hali tete

0

Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’

MUHIMBILI hali ni tete! Hayo ni maneno ya baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar baada ya kubaini kwamba kuna mashine za vipimo kadhaa hospitalini hapo zimeharibika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hospitalini hapo, umebaini kuwa kutokana na kuharibika kwa mashine hizo, sasa baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakitibiwa nje ya hospitali hiyo kubwa nchini.

Afisa mmoja hospitalini hapo ambaye alizungumza kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini kwa kuwa siyo msemaji, alisema vipimo vilivyoharibika kwa muda mrefu ni CT Scan na Mari Spaind ambavyo ni muhimu katika kupima magonjwa.

“Huu ni mwezi wa pili vipimo hivyo vikiwa vimeharibika, wagonjwa wanataabika sana na wengine wamekuwa wakienda hospitali binafsi kupimwa, lakini walio wengi wanashindwa kumudu gharama kwa kuwa ni kubwa,” alisema mtoa habari wetu.

Alisema kuna wagonjwa wanaotoka mikoani baada ya kupewa rufaa na wanapofika Muhimbili na kukuta hali kama hiyo, hukata tamaa.

Habari zinasema hata Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) nacho wataalam wake wanapata shida kutokana na mashine hizo kuharibika kwa kuwa wagonjwa wao walikuwa wakizitegemea.

Kaimu Ofisa Habari wa Muhimbili, Stephen John alipoulizwa alikiri kwamba mashine hizo ni mbovu.

“Hatua za makusudi zimechukuliwa kwa ajili ya kuzitengeneza na kazi hiyo  imepewa Kampuni ya Philips. Kasi ya kuzitengeneza ni kubwa na muda mfupi ujao zitafanya kazi,” alisema.

Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Afya Dk. Seleman Seif Rashid (pichani) ili afafanue tatizo hili lakini hakupatikana.

Leave A Reply