The House of Favourite Newspapers

Muhimbili ya sasa usipime!

0
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akitaza mashine ya CT Scanner.

 

IDARA ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, ni idara huru ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Ilianzishwa mwaka 2010, ikiwa na malengo ya kupunguza idadi ya wagonjwa ambao walikuwa wanapoteza maisha wakiwa mapokezi.

Awali, mgonjwa yeyote aliyefika au kufikishwa Muhimbili ilikuwa ni lazima apokelewe mapokezi kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo, kusajiliwa na kupelekwa wodini kwa ajili ya kusubiri huduma ambapo katika mchakato huo, wagonjwa wengi walipoteza maisha.

Kwa kuliona hilo kuwa ni tatizo, Muhimbili, ikishirikiana na serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau wa afya wakiwemo Abott Fund Tanzania, walianzisha idara hii kwa malengo ya kupunguza vifo vya wagonjwa.

Tofauti na awali, mgonjwa kufikia mapokezi, wagonjwa wote kwa sasa wanafikia kwenye idara hii kwa ajili ya kupewa huduma za haraka za kuokoa maisha yao.

Ili kuwafahamisha zaidi Watanzania juu ya kitengo hiki nyeti ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Gazeti la Uwazi limefanya mahojiano na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dk Juma Mfinanga ambaye anaelezea kwa kina juu ya huduma zinazotolewa kwenye kitengo chake.

UWAZI: Unapozungumzia magonjwa ya dharura na ajali unamaanisha nini?

Muonekano mudashara wa vyumba vya wagonjwa.

DK JUMA: Tunamaanisha mgonjwa yeyote yule anayefika au kufikishwa hospitalini akiwa na dalili hatarishi, viungo vyake au kujikuta katika hali inayosababisha mwili kudhurika baada ya kupata maradhi.

Dalili za magonjwa ya dharura ni mfano; mgonjwa anapopata malaria na isigundulike mapema au asipewe tiba nzuri na vijidudu vya malaria kuweza kuzaliana kwa wingi na kuathiri viungo vya mwili kama vile ubongo, figo au viungo vingine. Hiyo ndiyo tunaita dharura.

Kupoteza fahamu, kushindwa kupumua, kupata degedege, homa kali kwa watoto wadogo, kupoteza maji mengi ya mwili, viungo vya mwili kama figo kushindwa kufanya kazi, baada ya maradhi. Au watu wanaopata ajali wakiwa wazima kabisa, zote hizi ni dharura.

Dharura nyingine inaweza kuwapata akina mama wajawazito. Katika hali ya uzazi, wanaweza kupata tatizo, kama kuvuja damu nyingi au kupatwa na kifafa cha mimba. Haya ni baadhi ya mambo ambayo tunasema ndizo dharura. Ugonjwa wa dharura unaweza kumpata mtu yeyote bila kujali umri, jinsi wala uwezo wa kipato popote pale.

UWAZI: Kabla ya kuanzishwa kwa idara hii, hali ilikuwaje na baada, hali imekuwaje?

DK JUMA: Kabla ya kuanzishwa kwa idara hii wagonjwa wengi walikuwa wanafia mapokezi. Lakini kwa sasa idara imepunguza wastani wa asilimia tano ya wagonjwa wote waliokuwa wanafia mapokezi.

UWAZI: Idara ina uwezo wa kupokea wagonjwa wangapi kwa siku na kuwahudumia?

DK JUMA: Idara ina uwezo wa kupokea wagonjwa wa matatizo ya dharura 400 kwa siku na hii ni kutokana na miundo mbinu yake. Hata hivyo, idara hii ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa mahututi kati ya wastani ya watu 250 hadi 300 ambapo ni ongezeko la wastani wa watu 100, maana mwanzo wagonjwa wa dharura waliokuwa wanaweza kutibiwa haraka ilikuwa ni wastani wa 80 hadi 100 pekee.

UWAZI: Wakati wa nyuma, ili mgonjwa atibiwe kwenye Hospitali ya Taifa ilikuwa ni lazima apate barua kutoka Hospitali ya Rufaa, je, kwa sasa utaratibu wa kuwapokea wagonjwa wa dharura upo vipi?

DK JUMA: Katika hali ya kuokoa maisha ya mgonjwa, barua kutoka Hospitali ya Rufaa siyo ya msingi zaidi. Kwa hiyo, mgonjwa anaweza kupokelewa hata bila barua ilimradi yupo kwenye hali ya dharura. Tangu kuanzishwa kwake, idara imeshiriki kwenye majanga mbalimbali ya dharura. Baadhi yake ni ajali za meli zilizotokea miaka 2010, 2011, kuanguka kwa jengo kubwa jijini Dar, mwaka 2013, mafuriko ya maji pamoja na majanga mbalimbali yanayosababishwa na ajali za moto.

UWAZI: Ili kufika katika sehemu hizo ndani ya wakati, idara inatumia miundombinu gani?

DK JUMA: Kikubwa ni kwamba, kwanza, idara inatoa mafunzo ya mazoezi kila siku kwa kikosi maalum cha wataalam wanaokuwa tayari muda wote kwa ajili ya kutoa huduma sehemu yoyote ile. Lakini pia idara ina magari ya kisasa kabisa ya ‘ambulance’ ambayo mtu yeyote anaweza kuyahitaji kutoka mahali popote pale ndani ya Dar. Hata hivyo, ili huduma hii iwe endelevu, wahitaji wanachangia kiasi kidogo cha fedha kwa gharama ambazo zimewekwa na serikali.

UWAZI: Wagonjwa wengi wa dharura ambao idara inapokea ni wa magonjwa yapi?

DK JUMA: Wagonjwa wengi ni wa ajali za barabarani, wanafuata wagonjwa wa dharura za magonjwa ya moyo, magonjwa ya kuambukizwa kama vile malaria, homa ya ini, magonjwa ya upasuaji na kadhalika.

UWAZI: Wataalam wenu wanapata wapi mafunzo?

DK JUMA: Chuo cha Afya Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUASI), ndiyo kinachotoa mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa wataalam wa kada zote, kuanzia ngazi ya cheti hadi madaktari bingwa! Idara kwa kushirikiana na Taasisi ya EMATI, wanatoa elimu kwa watu kufahamu umuhimu wa kupata huduma mapema pale inapotokea wanapata matatizo.

UWAZI: Unatoa wito gani kwa jamii kuhusiana na magonjwa ya dharura?

DK JUMA: Jamii inatakiwa kufahamu kuwa, kwa sasa katika hospitali yake ya taifa, kuna kitengo maalum kinachoweza kuokoa maisha ya mtu anapotokewa na dharura ya ugonjwa wowote. Lakini jambo la msingi ni kuhakikisha mtu anapata huduma mapema iwezekanavyo pale tu anapohisi utofauti katika afya yake, ikiwa ni pamoja na kuwa na viashiria vya kupoteza maisha au viungo vya mwili.

Leave A Reply