MUHIMBILI YATOA TAMKO MTOTO ALIYEKATWA MKONO

SAKATA la mtoto Issaya Merikioni aliyechomwa sindano na daktari na kunyauka mkono kisha ukakatwa linaendelea; sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, imetoa tamko.

 

Tamko hili linahusu gharama za matibabu ya mtoto huyo ambayo mama yake amekuwa akidai kuwa aliambiwa na hospitali hiyo azilipe, jambo ambalo wengi ambao wamekuwa wakifuatilia habari ya mtoto huyo wamekuwa wakililalamikia.

 

Akizungumza na gazeti hili Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema: “Muhimbili kama Muhimbili hakuna kiasi chochote cha fedha alichotakiwa kulipia mzazi wa mtoto huyo hadi hapo alipofikia.

 

“Matibabu ya mtoto huyo yalisimamiwa na madaktari, nimefuatilia amefanyiwa bure hakuna malipo yoyote, kizuri zaidi oparesheni yake imefanyika salama.” Alipotafutwa mama wa mtoto huyo aitwaye Regina Hassan ili kuthibitisha kama kiasi cha shilingi laki mbili alichotakiwa kulipa kama gharama ya tiba kama alishakitoa alisema:

“Hapana; sijalipa fedha hizo. Nilitumia kiasi cha Shilingi 69,000 tu kwa ajili ya kununua dawa vichupa vitatu ambazo ni dawa zilizokuwa zimehitajika kwa haraka siku ambayo mtoto alienda katika chumba cha operesheni. ”Tangu nitumiea kiasi hicho cha fedha sijatoa pesa nyingine na dawa kama zile nilizonunua ninapatiwa kutoka kwa madaktari.”

Akizungumzia kuhusiana na hali ya Issaya alisema, kwa sasa anaendelea vizuri japo anapata maumivu makali yatokanayo na kitonda. Kisa cha mtoto huyo kukatwa mkono kilitokana na daktari mmoja katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kumchoma sindano mkononi kwa lengo la kumuongezea damu lakini ghafla mkono ulibadilika rangi na kukauka.

 

Kutokana na tatizo hilo yamekuwepo madai kuwa, huwenda daktari huyo wakati anataka kumuongezea damu alitoboa kimakosa mshipa wa kutoa damu safi kwenye moyo na kuacha wa kuingizia damu jambo ambalo linatajwa kusababisha tatizo lijulikanalo kitabibu kama Dry Gangrene.

 

Ni wazi kwamba, tangu mtoto Issaya apate mnyauko huo wa mkono hakukua na njia nyingine zaidi ya kupatiwa rufaa kutoka hospitali hiyo ya Morogoro na kuletwa Muhimbili jijini Dar es Salaam ambako  alikatwa mkono na kuanza maisha ya ulemavu. Kitendo hicho cha Issaya kukatwa mkono kimekuwa kikimsononesha mama yake na kuomba serikali iingilie kati ili daktari anayemtuhumu kufanya uzembe huo achukuliwe hatua.

 

Mbali na hilo, mama huyo amekuwa akiomba wasamaria wema wamsaidie misaada mbalimbali utakaowezesha mwanaye kupata chakula na yeye kuweza kujikimu kutokana na ukweli kwamba jijini Dar hana ndugu. “Uwazi lilimtafuta Waziri wa Afya Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ili kupata tamko la serikali kuhusu mtoto huo lakini hakuweza kupatika kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa. Aidha, hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu yake ya mkononi, hakujibu chochote.

Loading...

Toa comment