The House of Favourite Newspapers

Multichoice yawapeleka Watanzania sita kushuhudia Tamasha la Mama’s

Multichoice yawapeleka Watanzania sita kushuhudia Tamasha la Mama’s

KAMPUNI ya Multichoice Tanzania, imedhamini safari ya Watanzania sita kwenda nchini Afrika Kusini kwenye Mji wa Johannesburg kushuhudia Tamasha la Muziki la Mama’s.

Tamasha hilo ambalo litafanyika Oktoba 22, mwaka huu, litaoneshwa ‘live’ na chaneli za MTV Base na MTV zinazopatikana kwenye King’amuzi cha DSTV.

Katika tamasha hilo, Tanzania itawakilishwa na wasanii Navy Kenzo, Ali Kiba, Diamond, Rayvan, Yamoto Band na Vanessa Mdee ambao watakuwa wakishindania tuzo mbalimbali zilizopewa jina la MTV Africa Music Award.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande, amewataka Watanzania kuwaunga mkono washiriki wetu ili kuleta ushindi nyumbani.

“Watanzania tuwaunge mkono wenzetu ambao wanakwenda kutuwakilisha huko Afrika Kusini, tukiungana kwa pamoja naamini tuzo hizo zote wanazoshindania zitakuja nyumbani,” alisema Maharage.

Katika hatua nyingine, Maharage aliwataka wasanii wa filamu hapa nchini nao kuchangamkia fursa ya kuwania tuzo za Africa Magic Viewers Choice Award (AMVCA), ambazo zitafanyika Machi, mwakani.

Wanachotakiwa kufanya wasanii hao ni kutuma au kupeleka kazi zao kwenye ofisi za Multichoice Tanzania na mwisho wa kuwasilisha kazi hizo ni Oktoba 28, mwaka huu.

1.Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande (katikati) akizungumza na wanahabari katika mkutano huo.

2.Msanii wa Kundi la Navy Kenzo, Aika Mareale ‘Aika’ akizungumza jambo.

3.Baadhi ya wafanyakazi wa DSTV na wanahabari wakifuatilia mkutano huo.

Na Denis Mtima/Gpl

Comments are closed.