Mume Adaiwa Kumuua Mkewe kwa Kumchinja Kama Kuku

MARA: Wimbi la mauaji ya wanawake yanayofanywa na waume zao waliowapenda kwa dhati na kuahidi kuishi nao kwa shida na raha, linaendelea kutikisa kila kona nchini, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lina mkasa wa kusikitisha.

 

Katika hali ya kushtua, mwanaume Juma Marwa, mkazi wa Butiama, Mara, anadaiwa kumuua mkewe wa ndoa, Devota Boniface (16) kwa kumchinja kama kuku.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo la kutisha lilijiri baada ya mwanamke huyo kumuomba mdogo wake amletee beseni ili amnawishe mikono mumewe huyo kwa ajili ya kula chakula cha jioni.

 

Akilisimulia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA juu ya tukio hilo, kaka wa marehemu, Chacha Mwita alisema mdogo wake huyo aliyekutwa na umauti aliolewa na jamaa huyo yapata miezi nane tu iliyopita.

Alisema, siku ya tukio, ilikuwa yapata saa 2:00 usiku, familia hiyo ilipojumuika kwenye chakula cha jioni baada ya jamaa huyo kurejea nyumbani.

 

Alisema shemeji yake huyo aliporudi nyumbani, mkewe alimtengea chakula kisha akamuomba mdogo wake (mdogo wa mke) amletee beseni ili amnawishe mumewe.

“Kusema kweli hata kisa chenyewe kinashangaza maana mkewe alimuomba tu mdogo wake amletee beseni ili amnawishe mumewe.

 

“Hapo ndipo shemeji yangu akamwambia kwani amemuoa mdogo wake?

“Hicho tu ndicho chanzo cha yote kwani alianza kumshushia kipigo kabla ya kumchinja kama kuku,” alisema.

 

Alisema, wakati shemeji yake huyo akimsulubu, mkewe alikuwa akipiga kelele za kuomba msaada, lakini majirani walishindwa kufanya lolote kwa kumuogopa jamaa huyo ambaye zamani alikuwa mwanajeshi.

“Hakuna aliyejaribu kusogelea nyumba yao kwani wanamjua jamaa alivyo hatari. Kwa hiyo aliendelea kumkatakata mkewe mbele ya mdogo wake kisha akampigia simu mamamkwe wake na kumweleza kuwa ameshamuua mwanaye.

 

“Kiukweli ni tukio la kinyama sana kwa sababu mkewe alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu.

“Baada ya mauaji jamaa huyo alikimbilia msituni kujificha, lakini asubuhi alitafutwa hadi akapatikana.

“Alipokamatwa, alipelekwa Kituo cha Polisi cha Butiama na hadi sasa yupo mahabusu,” alisema kaka huyo wa marehemu.

 

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Daniel Shila alisema tayari mtuhumiwa amekamatwa na kinachofuata ni sheria kuchukua mkondo wake.

 

Stori: Gabriel Mushi, Ijumaa Wikienda 

 

MAZISHI YA MKE WA AGGREY MORRIS: MAMA Aishiwa NGUVU, WATOTO Watakuliza..!


Loading...

Toa comment