Mume afia ukweni kwake

KALI ya wiki! Mfanyabiashara maarufu jijini Dar, Jagna Issa (35), mkazi wa Magomeni-Mwembechai anadaiwa kufia ukweni na kifo chake kuacha viulizo baada ya maiti yake kukutwa ndani ya kisima cha maji kwenye nyumba ya mkwewe aliyetajwa kwa jina moja la Amina.

MJOMBA WA MAREHEMU ASIMULIA

Akizungumza na gazeti hili mapema wiki hii juu ya mkasa huo wa kusikitisha, mjomba wa marehemu Jagna, Ally Bilionea alisimulia kuwa, marehemu alikuwa akiishi Mwembechai lakini hivi karibuni aliugua malaria ndipo mkwewe, Amina akamtaka akaugulie kwake, Magomeni-Mikumi.

Mjomba mtu huyo alisema kwamba, wakati Jagna anaishi kwa mkwewe, mke wake Jamila aliendelea kuishi Mwembechai japokuwa hawakuwa na ugomvi.“Nakumbuka ilikuwa Jumatano ya wiki iliyopita. Nikiwa kwenye shughuli zangu za ufundi wa magari, nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu, akaniambia nyumbani kwa Jagna, Mwembechai kulikuwa na kilio.

MKE AANGUA KILIO!

“Ilibidi niende kule. Nilipofika, mke wa marehemu aliponiona alianza kuangua kilio akiniambia mumewe hajulikani alipo.
“Cha kushangaza, aliniambia Jagna alipotea saa moja iliyopita. Ilibidi nimuhoji inakuwaje aseme mtu amepotea kwa kutoonekana kwa muda mfupi kiasi hicho?

“Mkewe akasema kuna rafiki wa mumewe aitwaye Nairobi alimfuata Jagna ukweni wakafanya biashara ya fedha nyingi na kuondoka naye kwenye gari aina ya Toyota IST huku akiacha viatu vyake mlangoni,” alisema mjomba huyo.
Akiendelea kueleza kwa majonzi makubwa, mjomba huyo alisema kuwa, Jamila alidai kwa kuwa tangu Jagna ahamie kwa mkwewe hapo akiwa mgonjwa (japokuwa si mgonjwa wa kulala kitandani), hakuwa na kawaida ya kutoka ndiyo sababu iliyofanya aamini amepotea.

WAANZA HARAKATI ZA KUMTAFUTA

Mjomba huyo alisema ilibidi waanze harakati za kumtafuta kila kona ya Jiji la Dar kuanzia kwenye vituo vya polisi, hospitali na mitaani lakini bila mafanikio.

“Ilipofika Alhamisi, nilimwambia Jamila tukatoe taarifa Kituo cha Polisi cha Magomeni. Baada ya hapo tulikaa kikao cha familia kujadili jinsi ya kumpata ndugu yetu na hata tulipomuuliza Nairobi, alisema yeye alifanya biashara na Jagna kisha akaondoka huku jamaa akirudi ndani kwa mkwewe na kwamba, hakuondoka naye kama inavyodaiwa,” alieleza mjomba.

WAKUBALIANA KUCHUKUA POLISI

Alisema kuwa, baada ya kikao cha familia wakakubaliana siku iliyofuata (Ijumaa) wakachukue polisi, waende wakakague nyumbani kwa mkwewe alikokuwa akiishi Jagna kabla ya taarifa za kupotea.

SIKU YAFIKA
“Ilikuwa mishale ya saa moja asubuhi, Jamila alitoka chumbani huku akiongea na simu. Ghafla akaanza kulia na kuniambia Jagna amefariki dunia na maiti yake imekutwa kwenye kisima cha maji nyumbani kwa mama yake (Jamila).

“Tulipofika eneo la tukio, mimi niliwakuta kaka zake Jamila wakiwa katika zoezi la kuuopoa mwili wa Jagna kutoka kisimani. Wakati huo, Jamila yeye hakufika kuuthibitisha mwili wa mumewe badala yake alikwenda kwa ndugu wa mume kutaka awekwe eda. Mwili ulikutwa ukivuja damu.

MAJIRANI WATIA NENO
Kwenye eneo la tukio, baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo walipozungumza na gazeti hili walidai kwamba usiku walisikia mtu akipiga kelele ndani ya ukuta wa fensi ya nyumba hiyo lakini hawakuwa na namna ya kuingia kujua kulikoni.
Mjomba huyo alidai kwamba, walipowauliza kaka wa Jamila kwa nini wasisubiri polisi wafike ndipo wautoe mwili huo walisema walikuwa wanamuonea huruma marehemu.

BABA MKWE AONA MAITI
Alisema walipoulizwa waliuonaje mwili huo, walijibu kuwa baba mkwe wa Jagna, Mzee Yusuf (si yule wa Jahazi Modern Taarab) ndiye aliyeuona wakati anachota maji.

“Baada ya hapo tukaenda kuchukua polisi ambao walikuja kuuchukua mwili kwa ajili ya vipimo na taratibu za mazishi huku ndugu wa marehemu wakilalamika kutopewa majibu ya vipimo hivyo.Hata hivyo, mama na baba Jamila, Jamila mwenyewe na kaka zake walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Magomeni lakini mkewe aliachiwa siku iliyofuata huku simu zao zikishikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.

SIKU CHACHE ALINUNUA NYUMBA

Ndugu upande wa marehemu walidai kwamba, Jagna alikutwa na mauti ikiwa ni siku chache tangu aliponunua nyumba maeneo ya Mwembechai yenye thamani ya Sh. milioni 80.
Habari kutoka ndani ya Kituo cha Polisi cha Magomeni zilieleza kuwa, kifo hicho kina utata mkubwa hivyo kinahitaji uchunguzi wa kina.

KAMANDA ANASEMAJE?

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camilius Wambura alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa halijamfikia mezani kwake hivyo ameahidi kulifuatilia kwa kina na kulipatia majibu.
Marehemu Jagna alizikwa Ijumaa iliyopita kwenye Makaburi ya Magomeni, Dar. Mungu ailaze mahali pema peponi, roho yake. Amina.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Loading...

Toa comment