Mume Aliyeimkata Mikono Mkewe, Fundisho kwa Wanaume!

KAMA kuna habari iliyojaa mafunzo kwa wanaume ni hii ya Jackline Mwende ambaye alikatwa mikono yake na mumewe na habari yake kuandikwa na vyombo mbalimbali vya habari likiwemo Gazeti la National la Kenya baada ya mahojiano akiwa kijijini kwake Kathama. 

 

Ni habari iliyotikisa lakini nilipoisoma ilinifanya nisiwe mchoyo, nikaona nikuletee na wewe ambaye huenda hujawahi kuisikia. Mwanamke huyu alikatwa mikono na mumewe kwa madai kwamba hashiki mimba.

 

Lilikuwa ni jambo la kusikitisha kwa wananchi nchini Kenya lakini ni fundisho kwa wanaume wote duniani kwani baada ya kuachana na mwanaume huyo, Jack alipata ujauzito baadaye akazungumzia jambo hilo na kufichua siri.

 

Alikiri kwamba alikuwa na mpango wa kando baada ya mumewe kumuacha na alikatwa mikono na mume huyo siku tatu baada ya kushika mimba wakiwa wametengana na mumewe ingawa hawakuwa wametalakiana rasmi.

 

Habari kwamba Jackline Mwende ni mjamzito zilienea kwa kasi kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii nchini Kenya, ikizingatiwa kuwa alipata majeraha mabaya baada ya kushambuliwa na mumewe wa zamani kwa kutozaa.

 

Jackline alionyesha majeraha aliyopata kutoka kwa mumewe kwa kutozaa lakini alimpata mwanaume kutoka Kisii akawa rafiki yake wa karibu.

 

Habari yake kwamba amepata mimba iliwafanya Wakenya kupigwa na mshangao kwa sababu mumewe alimkata kwa upanga mikono yote miwili na kumuacha na majeraha mabaya kichwani hadi tunapoandika habari zake mwanamke huyo amekuwa hasikii, yaani ni kiziwi wa sikio moja; yote haya kwa sababu ya kutuhumiwa kuwa hazai.

 

Ilisemekana kuwa mumewe, Joseph Ngila ndiye aliyekuwa na matatizo ya kiafya ya kumtungisha mwanamke mimba, matatizo ambayo yangeweza kutibiwa. Sasa, Mwende amezungumzia ujauzito wake na akakiri alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na rafiki wa karibu lakini alikataa kutaja jina lake.

 

“Siku moja kabla nilionekana na baba wa mtoto niliyekuwa naye tumboni. Tulikuwa tukitafuta malazi mjini Machakos kwa sababu sikutaka kumleta nyumbani kwangu kwa kuwa aliyekuwa mume wangu tulishatengana.

 

“Nilikuwa naishi peke yangu kwa sababu mume alikuwa ameondoka nyumbani miezi mitatu awali. Kuna siku alikuja na kunishambulia kwa panga na kunisababisha matatizo makubwa ikiwemo kukatwa mikono,” alisema Jackline.

 

Aliongeza kuwa hana masikitiko yoyote kwa kuwa na mpango wa kando (mchepuko) kwani ndiye aliyechagua kufanya hivyo kwa sababu ya kutamani sana mtoto.

 

Wabunge wanawake pamoja na wahisani walimfuata mwanamke huyo ambapo Seneta Sonko aliahidi kumpa KSh 50,000 kwa yeyote atayemkamata mume huyo aliyefanya ukatili huo. Hata hivyo mwanaume huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

Kisa chake kiligutusha taifa nzima kwani kilikuwa cha aina yake na kudhihirisha jinsi dhuluma za kinyumbani zilizofikia kiwango hatari.

 

Mke wa Gavana wa Machakaos, Alfred Mutua, Lilian Nganga alikuwa msaada kwake wakati wote na kumuunganisha na wahisani ambao walifadhili matibabu yake kwa gharama za KSh10 milioni ili Jackline Mwende awekewa mikono bandia.

 

Kuonesha kuwa Mungu hamtupi mja wake, watu mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi wengine walimchangia kisha kumjengea nyumba ambapo ilifika wakati walimkabidhi nyumba iliyokuwa na vyumba vinne vya kulala pamoja na duka lililojaa bidhaa za kuuza.

 

Hata hivyo, amewashukuru wale wote waliomsaidia katika sakata lake ambalo limemkumba na kumfanya kupata kilema cha maisha.

NI FUNDISHO KWA WANAUME

Tukio la Jackline limekuwa likichukuliwa kama fundisho kwa baadhi ya wanaume Bongo ambao wamekuwa wakiwatuhumu wake zao kwa ugumba hata pale ambapo wao ndiyo chanzo cha tatizo.

 

Hivi karibuni kuliibuka mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii ishu kubwa ikiwa ni wanaume kupewa elimu ya kucheki afya zao kabla ya kuwatuhumu wake zao kwa kutoshika ujauzito.

 

“Niliwahi kusoma habari ya mwanamke mmoja kule Kenya ambaye mume wake alimkata mikono kwa kumtuhumu kutonasa mimba lakini kuonesha kuwa Mungu ni mkubwa, mwanamke yule alinasa mimba siku chache baada ya kuachana na mumewe. Hiyo inaonesha mume ndiye aliyekuwa na tatizo.

 

“Sasa jiulize mume wake huko aliko atakuwa anajisikiaje? Lile ni fundishio kubwa kwa wanaume na kwa wale ambao hawakuwahi kusoma habari ile naamini hii itawabadilisha,” aliandika kwenye Mtandao wa Instagram mdau mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Stella huku akiambatanisha na picha za Jack.

 

NENO LA UWAZI

Kwako mwanaume, ikiwa mkeo hapati mimba ni vema wote mkaenda hospitali kufanyiwa vipimo kwa sababu inawezekana mwenye matatizo ni wewe mwanaume. Hili ni jambo zito na tujifunze wote.

MAJERUHI WA AZAM HOI KITANDANI AZUNGUMZA – VIDEO

Loading...

Toa comment