The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 11

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Haa! Hutumii taulo shem?”

“Sipendi kabisa mama Kisu, sijui kwa nini?”

“Sasa wewe umesema huna mke, kanga unapata wapi huko nyumbani kwako?”

SASA ENDELEA NAYO…

“Jamani shem bwana, unanifurahisha!” nikasema.

Nilipotoa kauli hiyo mama Kisu akaniuliza nilikuwa ninamfurahisha kivipi, nikamwambia kuhusu swali lake la kwamba ninapata wapi kanga wakati sikuwa na mke nyumbani kwangu.

“Ndiyo je, wanaume wanaovaa kanga ni wale waliooa na huvaa kanga za wake zao sasa wewe unaponiambia kwamba hupendi kabisa kutumia taulo badala yake kanga ndiyo nakushangaa…”

“Shemeji yangu, basi mimi nipo tofauti kabisa na hao wengine, mimi nikijifunga kanga maungoni mwangu wakati nikienda kuoga au ninapokuwa nyumbani hasa chumbani najisikia vizuri sana.”

Kauli ya shemeji Tiaki ilizidi kunichanganya kwa sababu hata marehemu mume wangu mara kwa mara alikuwa akiniambia alikuwa anapenda sana kuvaa kanga akiwa nyumbani, tofauti iliyokuwepo kati yake na shem Tiaki ni kwamba Tiaki hakuwa na mke.

“Haya shem, tuachane na mambo ya kanga kwani kuna taarifa nimepata imenishtua sana nataka unishauri maana nipo njia panda,” nikamwambia.

“Taarifa gani tena mama Kisu?” Tiaki akaniuliza.

Nilimsimulia kila kitu kuhusu yule mtu aliyenipigia simu na kujitambulisha kama alikuwa ni mfanyakazi mwenzake marehemu mume wangu, Tiaki akashtuka na kuniuliza kama ni kweli niliyomueleza.

“Sasa shemeji jamani mimi nikudanganye wewe ili iweje kwa mfano? Tena mtu huyo kajitambulisha kwamba anaitwa Simon na ni mfanyakazi wa Kampuni ya Power Domestic Material ambayo mume wangu alikuwa akifanyia kazi,” nilimwambia Tiaki.

Nilipomwambia hivyo, Tiaki aliinuka kisha akaniuliza kama mle ndani mlikuwa na maji ya baridi sana ya kunywa, nikamwambia yalikuwepo akasema nikamletee yawe kwenye jagi.

Aliponiambia hivyo, nilishtuka kwani hata marehemu mume wangu enzi za uhai wake nilipomshirikisha kuhusu jambo lolote tata na kumuomba ushauri, alikuwa akisimama na kuomba nimpe maji ya baridi sana.

“Mhh! Huyu Tiaki mbona yuko hivi, huyu atakuwa siyo mtu mwema kwangu,” niliwaza.

Hata hivyo, kila nilipokumbuka zawadi alizoniletea na maongezi yake nikawa nafuta kauli ya kwamba siyo mtu mwema kwangu na kumuona alikuwa mtu wa kawaida.

“Mama Kisu, mbona nakuona kama uko mbali unawaza nini?” Tiaki alinishtua.

“Hapana shemeji yangu, ngoja nikakuchukulie maji uliyoomba,” nilimwambia huku nikielekea jikoni.

Kule jikoni bado niliendelea kumfikiria Tiaki na mambo aliyokuwa akiyafanya ambayo yalishabiiana kwa kiasi kikubwa na ya marehemu mume wangu, mfano kitendo cha kupenda kuvaa kanga na kunywa maji ya baridi sana nilipomuuliza kuhusu mambo tata.

“Mh! Kweli hii dunia ina mambo ya kustaajabisha,” nilizungumza peke yangu kule jikoni.

Nilipojaza maji kwenye jagi, nikachukua glasi na kuelekea chumbani kwangu nilikomuacha Tiaki, ile naingia nilimuona akiwa ameshika kioo anajitazama usoni, nilishtuka sana.

Kilichonishtua ni kwamba tabia hiyo ya kujiangalia kwenye kioo alikuwanayo pia marehemu mume wangu, nikiwa nimesimama aliniambia niliweke lile jagi kwenye meza ya kujipambia iliyokuwa mbele yake.

Nikiwa nashangazwa na mambo ya Tiaki, alipomaliza kujitazama kwenye kioo alinishukuru kwa kumletea maji kisha akaniuliza kama mle ndani mlikuwa na kikombe kikubwa cha plastiki.

Aliponiambia hivyo, moyo wangu ulipiga pa kwani hata marehemu mume wangu   alikuwa anapenda sana kutumia kikombe kikubwa cha plastiki alipotaka kunywa maji, nikamwambia kilikuwepo.

“Naomba niletee shemeji yangu, mimi huwa sipendi kabisa kutumia glasi kunywea maji naona zinanichelewesha,” Tiaki aliniambia.

Kauli ya shemeji Tiaki iliniweka katika wakati mgumu sana maana hata mume wangu alikuwa akipenda kuniambia hivyo, nikabaki nikimwangalia.

“Vipi mama Kisu, mbona naona kama kuna jambo linakutatiza?” Tiaki aliniuliza.

Kwa vile nilitaka kumfuatilia kwa karibu kuhusiana na tabia yake iliyofanana na marehemu mume wangu nilimdanganya kwamba hakukuwa na jambo lolote.

“Hapana shemeji yangu, unaonekana dhahiri una kitu kinakusonga, kuwa huru kuniambia maana tangu nilipoomba uniletee kikombe kikubwa cha plastiki cha kunywea maji umepoa ghafla,” Tiaki aliniambia.

“Hakuna tatizo shemeji, ngoja nikachukue,” nilimwambia.

Je, nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply