ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Hapana shemeji yangu, unaonekana dhahiri una kitu kinakusonga, kuwa huru kuniambia maana tangu nilipoomba uniletee kikombe kikubwa cha plastiki cha kunywea maji umepoa ghafla,” Tiaki aliniambia.
“Hakuna tatizo shemeji, ngoja nikachukue,” nilimwambia.
SASA ENDELEA MWENYEWE…
Kwa kweli nilikwenda jikoni huku nikiwa nashindwa kumuelewa Tiaki, nikaamua kumpigia simu wifi yangu lakini nikakumbuka simu niliiacha chumbani alikokuwa Tiaki. Nilichukua kikombe na kurejea chumbani na kumkabidhi Tiaki ambaye alisema asante ndipo alifungua jagi lililojaa maji akayamimina hadi kujaza kikombe.
Wakati huo nilikuwa ninamwangalia kwa makini ndipo alikinyanyua kile kikombe na kukipeleka kinywani, alikunywa maji yote bila kupumzika, nikaachama kwa mshangao. Nilipatwa na hali hiyo kwa sababu hata mume wangu alikuwa akinywa maji kwa mtindo huo nikajikuta namuuliza Tiaki kama hakuwa akinifanyia mchezo wa kiini macho.
“Mchezo wa kiini macho kivipi mama Kisu?” aliniuliza huku akiniangalia kwa macho yenye uelewa mkubwa.
Nilimwambia haiwezekani kila kitu alichofanya kifanane na marehemu mume wangu kwa kiasi kikubwa. Tiaki alicheka sana kisha akaniangalia akisema:
“Mama Kisu bwana na huyo mume wako, sasa mimi nikufanyie kiini macho ili nipate faida gani na kwa nini kwanza? Au unataka kuniambia unaniona mimi ni jini siyo?”
Nilishtuka aliposema hivyo kwani ni ukweli kwamba mimi nilikuwa namuona Tiaki ni jini aliyeamua kunichezea kwa kutumia staili za tabia zote za marehemu mume wangu baba Kisu.
“Hapana shemeji, sema tu nashtuka kwa sababu mambo yako yananikumbusha mume wangu au niseme rafiki yako, baba Kisu,” nilisema ili kumpoza asije akaniua kwa kuninyonya damu bure maana nilisikia ndivyo majini yanavyofanya.
Ghafla lilinijia wazo kwamba ni kwa nini nilikubali Tiaki awepo chumbani na mimi niwepo chumbani? Kimaadili mimi na yeye hatukufikia huko, ilikuwa bado.
“Shemeji niko sebuleni,” nilimwambia huku nikitoka.
Tiaki alinishika mkono, akaniambia nikae kitandani, nilikaa kisha na yeye akakaa pembeni yangu. Alinishika mgongoni na kuniambia anaomba atakachokiongea nikisilikilize kwa umakini wa hali ya juu sana.
“Sawa,” nilimjibu.
“Mimi nimeshasema nataka wewe uwe mke wangu. Kwanza napenda kukwambia kwamba, sitanii katika hilo na wala sina nia mbaya na wewe.
“Sikuwahi kukutamani wakati ukiwa na rafiki yangu lakini kwa sababu hayupo na mimi nimeshakuwa na nia ya kuoa, nimeona wewe unafaa. Au nasema vibaya mama Kisu?”
“Husemi vibaya shemeji. Ila mimi sijakuamini,” niliamua kumfungukia ili nione.
“Kivipi mama Kisu?”
“Kutoka moyoni, sikuoni kama wewe ni mwanaume mzuri kwangu.”
“Una maana naweza kukuua au mimi ni tapeli?”
“Unaweza kuniua,” nilimwambia huku nikimtazama.
“Kivipi?”
“Mimi kusema ukweli hata ukiamua kuniua sasa hivi hapa lakini kutoka moyoni ninavyojua wewe ni jini!”
Nilimwona Tiaki akijishika kichwa na kujikuna kisha akaniangalia, akanisogelea karibu, akanishika tena mkono na kuniambia:
“Hujanitendea haki mama Kisu. Siamini kama ulifikia hatua ya kunifikiria vibaya kiasi hicho. Mimi si jini na wala sina harufu ya jini. Mimi mwenyewe nimekuwa nikisikia kwenye simulizi kwamba kuna majini.”
Alipomaliza kusema hivyo, niliinua uso na kumwangalia, nikajisikia dhamira ikiniumiza, nikamwomba msamaha:
“Samahani sana shemeji, nilijikuta nikisema hivyo tu ili niweze kuwa huru na amani ndani ya moyo wangu. Lakini napenda kukwambia kwamba, kuanzia leo nimeamua kukuamini. Kama kweli ungekuwa na ubaya na mimi, ungekuwa umeshaniua.”
“Ndiyo hapo sasa mama Kisu. Halafu kama kweli mimi ni jini, ningekuwa hadharani hivi?”
“Nisamehe sana shemeji Tiaki,” nilirudia kusema.
Tiaki aliniangalia kwa macho yaliyojaa shauku ya jambo fulani kisha akanishika, akanisogezea kwake, nikasogea.
“Mama Kisu,” aliniita kwa sauti ya chini sana.
“Bee.”
“Nakupenda sana.”
“Nashukuru sana kwa kunipenda.”
“Naomba nikubusu.”
Nilimtegea shavu, akanibusu! Kisha tukabaki tunatazamana bila kusema lolote. Si yeye wala si mimi.
“Mama Kisu,” aliniita tena.
“Bee,” na mimi nilimwitikia tena.
“Nakupenda tena.”
“Nashukuru sana sana na sana.”
Ghafla nilimwona ananikumbatia halafu akanielekeza kulala kitandani, nikaelekea hapo polepole huku mapigo ya moyo yakinienda kwa kasi ya ajabu.
“Shemeji Tiaki,” niliita.
“Naam.”
“Unataka kufanya nini?”
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili wiki ijayo.