The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili – 9

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

“Ila sasa kuna jambo moja shemeji. Wewe kuwa jasiri, usiyumbishwe. Achana kabisa na zile habari za yule shemeji yako wa kijijini, Daniel. Usimuwazie kabisa, we  niwazie mimi tu.”

Palepale simu ilidondoka chini kutoka kwenye mkono wa kulia.

SASA ENDELEA MWENYEWE:

Niliiangalia ile simu pale chini, nikaogopa hata kuishika maana Tiaki aliniambia jambo la ajabu sana. Nilijiuliza yeye alijuaje kuhusu uwepo wa Daniel! Na kwa nini aseme niachane naye, yeye anajua kuna nini kati yetu.

Pale chini, simu ilisambaratika kwa maana kwamba, ilitoka mfuniko, ikatoka hadi betri. Niliiokota na kuiunga tena kisha nikaiwasha, simu ya Tiaki ikaingia palepale, moyo wangu ukasema pokea, nikapokea.

“Tatizo lako wewe mama Kisu unaniwazia vibaya. Mimi si mtu mbaya kwako. Nataka ndoa kwa sababu najua haupo kwenye ndoa tena. Nipe nafasi.”

“Nina swali moja Tiaki.”

“Niulize mama Kisu.”

“We umejuaje nina shemeji anaitwa Daniel na nina matatizo naye?”

“Mama Kisu bwana. Kwani nilipokuwa kwako, ukaingia chumbani kuongea na wifi yako si mlimzungumzia Daniel? Maana kumbuka mlango ulikuwa wazi. Halafu siku ile kwenye basi wakati tunakuja, basi liliposimama abiria kujisaidia si uliongea na shemeji yako kuhusu Daniel?”

“Mh! Wewe Tiaki wewe. Haya kwenye basi ulisikiaje?”

“Si nilisimama nje ya dirisha ulilokaa kwa chini. Nikawa nasikia kila kitu.”

Nilikubaliana na Tiaki lakini nikawa sina kumbukumbu kama ni kweli nilipoingia chumbani niliacha mlango wazi na sikukumbuka kama kwenye basi, yeye alisimama nje, kwa chini ya dirisha.

“Sawa, sasa unasemaje Tiaki?”

“Nataka ndoa na wewe mama Kisu.”

“Mbona ghafla sana Tiaki. Yaani kumaliza arobaini tu unataka ndoa na mimi! Jamani!” nilimlalamikia Tiaki.

“Najua, ndiyo maana nikasema nakuachia umwombolezee mumeo kwanza mpaka utakaposema mwenyewe sasa basi.”

“Sawa, basi niache mpaka nitakapokujibu.”

Tiaki alikata simu, nikaenda kukaa kitandani. Nilikuwa nawaza mawili matatu kuhusu huyu mwanaume Tiaki. Ni kwa nini ana tabia zinazomwonesha si mtu mzuri lakini anazipangua vizuri?

*   *   *

Miezi miwili ilikatika, nilikuwa bado namfikiria Tiaki kila mara. Hakuwahi kunipigia simu wala kunitumia meseji tangu nilipomwambia nitamjulisha. Sikuwahi kumwambia wifi kuhusu Tiaki na nia yake ya kutaka kunioa.

Siku hiyo, nikiwa nimejilaza nje kibarazani, nikajisikia kumtumia meseji ya kumuuliza maendeleo yake.

“Mimi naendelea vizuri mama Kisu. Nilikwenda Arusha, Kagera, Mwanza na Nairobi, nimerudi jana tu.”

Nilikuwa nimelala lakini nilijikuta nikiamka na kukaa kwenye mkeka. Ni kwa sababu ya kumsikia Tiaki akisema alikwenda Arusha, Kagera, Mwanza na Nairobi. Hizo sehemu mara nyingi alipenda kwenda mume wangu, baba Kisu, sasa nilishtuka sana kumsikia huyu naye eti alikwenda huko.

“Kikazi?” nilimuuliza.

“Ndiyo mama Kisu.”

“Mh!” niliguna mwenyewe. Nikamuuliza:

“Umetuletea zawadi gani?”

“Zawadi nyingi tu mama Kisu. Nimekuja na mafuta ya losheni, vitenge na sabuni za kuogea.”

Nilisimama na kwenda ndani, chumbani kabisa. Nikapiga magoti na kusali nikimwambia Mungu, kama Tiaki ni marehemu mume wangu amekuja kwa sura nyingine aniambie. Nilisema hivyo kwa sababu, vitu alivyosema Tiaki amekuja navyo kutoka safari ndizo zawadi alizokuwa akija nazo mume wangu. Losheni, sabuni za kuogea na vitenge.

Wakati nikiendelea kusali, meseji ikaingia kwenye simu, niliacha kusali ili niisome.

“Mama Kisu nikuletee zawadi zako kama hutajali?”

Nilijikuta nikisema niletee baba!! Nitashukuru sana!

Basi, lakini nikaendelea kumfikiria Tiaki si mtu mzuri. Niliwaza hata kule kumtumia meseji baada ya miezi miwili na akasema amerudi jana yake ni nguvu zake mwenyewe.

Ndani ya dakika kumi na tisa hivi, maana nilikuwa nahesabu, Tiaki alifika nyumbani kwangu akiwa amebeba begi kubwa kiasi. Nilitoa macho pima! Kwa sababu ndivyo mume wangu alivyokuwa akiingia kutoka safari, vitu vyake alivibebea ndani ya begi.

Nilimpokea huku nikitetemeka sana. nilimwangalia kwa hofu na wasiwasi.

“Karibu sana,” nilimwambia.

“Asante sana mama Kisu. Za hapa?” aliitikia huku akikaa kwenye kochi dogo na kuniangalia.

“Hapa kwema sana, nashukuru sanasana kwa zawadi, Mungu akubariki sana jamani,” nilimwambia, akasema atubariki wote. Yaani huyo Mungu.

Nilimkaribisha juisi kisha nikaenda chumbani kupeleka lile begi. Nililifungua na kutoa vitenge pea tano, sabuni nyingi tu, kama thelathini na chupa za losheni tano.

Nikiwa bado chumbani ghafla mlango ulisukumwa, akaingia mtu, nikashtuka na kumwangalia.

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Leave A Reply