The House of Favourite Newspapers

MUNA ABURUZWA POLISI NA MAMA’KE

Image result for MUNALOVE
Rose Alphonce Nungu ‘ Muna Love’

BADO mambo ni moto! Mama mzazi wa mwigizaji wa filamu za Kibongo, Rose Alphonce Nungu almaarufu Muna Love, Ritha Rabia Moyo amefikia hatua ya kumburuza Polisi mwanaye huyo kwa makosa ya mtandaoni ya kumtukana na kumkana yeye na mtoto wake.  Muna alidaiwa kumkana mzazi wake huyo kisha kugombana naye baada ya kudai hana mtoto mwingine zaidi ya marehemu Patrick Peter, jambo ambalo ndugu zake walidai si kweli kwani ana mtoto mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 13.

Juzi, Jumatatu, mzazi huyo pamoja na ndugu wa karibu walitinga kwenye Kituo cha Polisi cha Kawe jijini Dar kisha kumfungulia Muna mashitaka hayo.  Akizungumza na Risasi Mchanganyiko juu ya sakata hilo, mmoja wa ndugu hao wa Muna aliyeomba hifadhi ya jina alisema: “Tulikwenda Kituo cha Polisi Mabatini (Kijitonyama) ambapo tulitakiwa kuripoti kutokana awali Muna kumshtaki mama yake.

“Baada ya hapo mama alikwenda kumshitaki Muna katika Kituo cha Polisi cha Kawe kwa makosa mawili ambayo ni kumtukana na kumkana yeye pamoja na mjukuu wake huyo aliyeko Moshi mkoani Kilimanjaro. “Pale Kawe tulipewa RB ya kumkamata Muna namba KW/ RB/6644/2018- MATUMIZI MABAYA YA MTANDAO. “Baada ya hapo tulipewa askari, tukafika nyumbani kwa Muna maeneo ya Mbezi- Jogoo (Dar).

“Hata hivyo, tulimkosa Muna kwa kuwa hakuwepo nyumbani hivyo ikashindikana kumkamata, lakini bado anaendelea kusakwa na Polisi popote alipo.” Alipotafutwa mama Muna kuhusiana na ishu hiyo ya kumshtaki mwanaye alikiri kwamba ni kweli na anasakwa na jeshi la polisi kwani juzi (Jumatatu) walimfuata nyumbani kwake hawakumkuta.

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Muna lakini hazikuzaa matunda kutokana na simu yake ya mkononi kutokuwa hewani. Muna amekuwa kwenye mgogoro na mama yake tangu alipodai mzazi wake huyo alishafariki dunia wakati yupo hai.

STORI: Neema Adrian, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.