The House of Favourite Newspapers

Muna Aibua Mapya Mavazi ya Mwanaye

Msanii Rose Alphonce ‘Muna’

KISHINDO kifo cha mtoto wa msanii Rose Alphonce ‘Muna’, Patrick Peter kingali kikivuma na kusababisha mapya kila uchwao, safari hii mavazi yake yamehusika.

Mama mzazi wa mtoto huyo ambaye ni marehemu amejitokeza tena hivi karibuni na kulieleza Wikienda kwa njia ya simu kutoka Kenya kwamba mavazi ya mwanaye hayatagawanywa kwa utaratibu uliozoeleka.

 

KWA NINI MAVAZI?

Ishu ya mavazi iliibuka hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii na hasa baada ya kuwepo kwa madai kwamba Patty amefariki na kuacha mavazi lukuki yenye thamani ambapo watu walijiuliza yatagawanywa kwa akina nani?

Kwa mujibu wa watu wa karibu na Muna wanasema kwamba mtoto huyo mbali na kuwa na nguo za bei mbaya ana vito, viatu, saa za mkononi, pete na kila aina ya urembo wa gharama.

Uwepo wa taarifa hiyo ulilifanya Wikienda limtafute Muna na kumuuliza vitu vya marehemu vitagawiwa kwa utaratibu gani na akina nani watahusika kwenye urithi huo?

 

UTARATIBU WA KUGAWA MAVAZI YA MAREHEMU UKOJE?

Desturi za jamii mbalimbali hapa nchini ambazo zimekuwa zikifuatwa pia na baadhi ya waumini wa dini; mtu akishafariki mavazi yake husubiri kwa siku arobaini na kisha hutolewa na kugawanywa kwa ndugu wa karibu.

Utamaduni huu ndiyo uliowasukuma baadhi ya wachangia hoja kwenye mitandao ya kijamii kuibua mjadala wa nini kitazingatiwa kwenye ugawaji wa mavazi ya Patty ambapo utata wa baba wa mtoto ungali unaishi.

 

“Hata kama ana kabati kumi za nguo zitagawanywa kwa ndugu.”

“Atakayesimamia ugawaji huo ni Peter (Zacharia) au Casto (Dickson)?”

“Muna mwenyewe na Joel Lwaga atahusika.” Baadhi ya majibizano ya hoja mitandaoni.

 

MSIKIE MUNA SASA

Pamoja na kuwepo kwa taarifa kwamba Muna ameshaachana na habari za msiba wa mwanaye na kwamba yuko nchini Kenya akila bata, Wikienda lilifanikiwa kuzungumza naye kama ifuatavyo:

WIKIENDA: Habari za Kenya?

MUNA: Nzuri za kwako?

WIKIENDA: Huku kwenye mitandao ya kijamii kuna mambo mengi kweli kuhusu wewe, sipendi kukukumbusha machungu ya msiba lakini isaidie jamii kujua huko Kenya unafanya nini?

MUNA: Niko huku nafanya ushuhuda wa neno

la Mungu pamoja na yale niliyopitia.

WIKIENDA: Mbona mapema sana, watu wanasema si ungesubiri hata arobaini ya mwanao ipite ndiyo ufanye mambo hayo?

MUNA: Mimi ni Mkristo mambo ya arobaini siyajui, ninachojua ukimaliza kuzika unaendelea na maisha yako huku ukimtukuza Mungu kwa kutimiza mapenzi yake.

WIKIENDA: Sasa hii ishu ya mavazi ya mwanao mtaifanya lini maana jamii ilitaraji pengine kugawa nguo zake kungefanyika siku ya arobaini yake ambayo wewe huiamini, itakuwaje?

MUNA: Mavazi ya mwanangu hayatagawanywa kwa utaratibu huo, marehemu aliacha maono na vitu vyake vitakwenda sawa na maono aliyoyaacha.

WIKIENDA: Maono aliyoacha Patty! Maono gani hayo tena?

MUNA: Mwanangu alikuwa na maono mengi sana, alikuwa ni wa kipekee; mimi siwezi kukuambia leo nini kitafanyika kwenye mavazi na vitu vyake, nimepanga kuzungumzia hili siku chache zijazo, naomba usubiri.

MAONO YA PATTY NI YAPI?

Kama ambavyo wewe msomaji unajiuliza ndivyo Wikienda linavyojiuliza hasa baada ya Muna kusita kueleza wazi maono hayo na hivyo kuacha maswali yasiyo na majibu.

Hata hivyo, Wikienda lilipotoka nje ya boksi na kuwatafuta baadhi ya ndugu wa karibu wa Muna ili waelezee wanachokijua kuhusu maono ya Patty juu ya urithi wa mavazi yake, uwazi haukupatikana.

“Kama alivyokuambia mzazi subiri utaambiwa yote na mimi nakushauri usubiri, lakini kuhusu nguo Patty anazo nyingi sana,” alisema ndugu wa Muna ambaye jina linahifadhiwa.

MAJIBU YA KULA BATA KABLA YA AROBAINI

Sahani tupu haitowezwi tonge; baada ya ukweli wa maono kukosekana Wikienda lilimfikishia Muna tuhuma mpya kwamba:

“Ameanza kujiachia mapema mno baada ya kifo cha mwanaye na hizo nguo anazovaa na hasa suruali haziendani na imani yake.”

Majibu ya Muna yalikuwa hivi:

“Kuna kitu nitaposti (kwenye mitandao ya kijamii) watu watajua.”

Aidha baada ya kujibu hivyo Wikienda lilifanikiwa baadaye kuziona posti nyingi kwenye Instagram yake ambayo Muna aliandika kwa kirefu kuelezea kuwa hawezi kumfurahisha kila mtu na kwamba anachozingatia ni kumtumikia Mungu.

ISHU YA DNA YAFUKUTA

Kitu kingine ambacho kinaonekana kuwa mjadala wake haujafungwa ni kuhusiana na baba mzazi wa mtoto huyo ni Casto kama anavyosema Muna au ni Peter anayetamba kuwa vielelezo vyote kuwa baba wa Patty anavyo.

Wachache kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakiufikisha mbali mjadala huu kwa kuandika posti zao kuwa:

“Kama kila mtu anajihalalisha basi kaburi likafukuliwe vipimo vya DNA vihusike kumaliza utata.

Wikienda lilijaribu kumuuliza mmoja kati ya ndugu wa Peter juu ya hoja ya kufukua maiti na kwenda kupima DNA ambapo alisema, anayebisha ndiye aende akafukue siyo wao.

“Labda huko kwa akina Muna ndiyo wanaona kuna utata wa baba wa mtoto, sisi huku hatuuoni, kama ni kupima DNA waende wao,” alisema dada wa Peter ambaye hakupenda kuandikwa jina.

Patty alifariki Julai 3, mwaka huu nchini Kenya alikokuwa akipatiwa matibabu ya uvimbe kwenye ubongo.

Comments are closed.