The House of Favourite Newspapers

MUNA LOVE: HATA UNGEKUWA WEWE UNGEOKOKA TU!

SUALA la wasanii na watu maarufu kutangaza kuacha maovu na kumrudia muumba wao si geni. Kwa hapa Bongo wapo wengi ambao wamewahi kufanya hivyo ambapo miongoni mwao ni wanamuziki Suma Lee, QJ, Mzee Yusuf na wengineo.

Lakini pia katika orodha hiyo wapo waigizaji ambao ni pamoja na Mainda, Anti Lulu na Jimmy Mafufu.

 

Wapo ambao huweza kudumu katika wokovu huo na wapo wengine ambao shetani huwavuta shati na kujikuta wakirudi kwenye himaya yake. Matukio yote hayo yanasogeza siku za maisha mbele!

Sasa, katika miezi ya hivi karibuni, mwanadada mwigizaji ambaye alipata umaarufu zaidi kutokana na kuwa swaiba wa karibu wa kipenzi cha Watanzania wengi, Wema Isaac Sepetu, Muna Love alitangaza kuokoka na kumrudia muumba wake.

 

Tangu atangaze hilo, ukimuona Muna, kama ulikuwa unamfahamu unaweza kufikiri ni watu wawili tofauti, kati ya yule uliyekuwa unamjua huko nyuma na unayemuona hivi sasa.

Kuanzia zungumza yake, tembea yake na hata vaa yake, ipo kiwokovu na kiukweli amebadilika mno. Lakini pia tangu aokoke amekuwa kimya sana kwenye media, bila shaka wasomaji mngependa kufahamu maisha yake mapya kwa sasa. Over Ze Weekend imemtafuta na hapa anafunguka kila kitu!

 

Over Ze Weekend: Muna nini kimebadilika zaidi kati ya maisha yako ya awali na sasa?

Muna: Vingi sana vimebadilika. Kuanzia utaratibu wa maisha yangu ya kila siku, siendi tena kwenye sehemu za starehe kama ambavyo ilikuwa awali, sinywi tena pombe, sijichanganyi na marafiki wale niliozoea kuwa nao mara kwa mara. Kiukweli kwa sasa ninaishi maisha mengine kabisa na yenye furaha na amani.

Over Ze Weekend: Kuna mashabiki wako hawafahamu una muda gani kwenye wokovu na kipi kilikufanya hasa kuchukua uamuzi huo?

 

Muna: Nina miezi mitano. Aliyenisababisha hasa niokoke ni mwanangu Patrick.

Over Ze Weekend: Ilikuwaje?

Muna: Unajua Patrick aliugua kwa muda mrefu miguu. Na ugonjwa wake ulianza kama utani. Tuliamka siku moja akawa hatembei. Anatambaa tu. Nilijua anatania, lakini hali iliendelea kuwa siriaz. Nikampeleka Hospitali ya Agha Khan, akafanyiwa vipimo nikaelezwa ana maumivu tu baadaye atakuwa sawa. Lakini bado hakupona.

 

Nikampeleka tena Hospitali ya Sanitarian akafanyiwa uchunguzi ndipo wakaniambia nimpeleke Muhimbili kwa uchunguzi zaidi. Muhimbili, baada ya kumchunguza walimfanyia oparesheni na kumuwekea vyuma kwenye mapaja huku wakiniambia anatakiwa kuongezewa madini ya ‘calcium’.

Lakini baada ya muda vile vyuma vikawa vinatunga usaha. Ikabidi wafanye oparesheni ya pili na baadaye ndipo wakafanya oparesheni ya tatu na kumuwekea madini hayo. Madaktari wakaniambia baada ya kuangalia maendeleo yake, atatakiwa tena kufanyiwa oparesheni ya nne na ya mwisho ambayo ndiyo ingem-saidia kurudi kwenye hali yake ya kutembea, lakini ingegharimu kati ya shilingi milioni 25 hadi 50.

 

Over Ze Weekend: Aisee pole sana. Enhee ikawaje?

Muna: Nilihisi kuchanganyikiwa. Zilikuwa ni pesa nyingi ambazo nilifahamu kuzipata kwa haraka ulikuwa ni mtihani mzito. Lakini jambo la kushangaza wakati mimi ninaumiza kichwa juu ya fedha hizo, mtoto yeye kila mara alikuwa ananiambia tu kwamba mama ukiokoka, basi mimi ninapona.

Aliendelea kuniambia hivyo kwa siku kadhaa na kuna wakati hata akina mama niliokuwa nao pale hospitalini (Muhimbili) walikuwa wakiniambia usiku nikipitiwa na usingizi Patrick alikuwa anazungumza peke yake na kudai kwamba anazungumza na malaika.

 

Over Ze Weekend: Uliwahi kumuuliza juu ya hilo?

Muna: Ndiyo. Alisema hivyohivyo na kunisisitiza niokoke. Baada ya kuona ananisisitiza zaidi, niliamua kuokoka kweli. Nilitafuta mchungaji, akaja Muhimbili na kutuombea. Nikatubu na kuokoka.

Over Ze Weekend: Baada ya kuokoka kweli akapona?

Muna: Alipata nafuu. Na jambo la kumshukuru Mungu, ile oparesheni ya nne haikuweza kufanyika. Badala yake madaktari waliniambia niende naye nyumbani. Lakini niishi naye kwa uangalifu kwa muda na hakuwa anaruhusiwa kukanyaga chini.

 

Over Ze Weekend: Ana umri gani na ungeweza kuishi naye vipi bila kukanyaga chini?

Muna: Patrick ana umri wa miaka saba. Na suala la kuishi naye bila kukanyaga chini hata mimi lilinipa shida sana. Lakini kuna machuma walimfungia ambayo yalimsaidia kuwa juujuu.

Over Ze Weekend: Nini kiliendelea hadi akapona?

Muna: Baada ya kurudi nyumbani, nikiwa sipo, nikirejea nyumbani msaidizi wa kazi alikuwa ananiambia kwamba nikitoka Patrick naye anatoka kwenye machuma na kutembea. Ilinishangaza na nikawa mkali kidogo katika hilo, lakini siku moja aliniambia nikimpeleka kanisani atapona kabisa na alinisisitiza sana.

 

Nikaamua kufanya hivyo. Nikampeleka kwenye kanisa linaloitwa Dokas. Tulivyofika pale kanisani alipoiona tu picha ya Yesu, akaanza kutembea. Na huo ndiyo ukawa uponyaji wake. Kwa hiyo kuanzia hapo nikaamua kuokoka kwelikweli. Maana kwa haya hata mtu yeyote angeokoka tu!

Over Ze Weekend: Vipi lakini baba mtoto Casto Dickson amekuwa akikusaidia katika kipindi chote hicho kigumu?

Muna: Kuhusu Casto siwezi kuzungumza lolote?

Over Ze Weekend: Kwa nini? Umeokoka zungumza tu ukweli.

 

Muna: Ukweli nitakaouzungumza utakuwa haujengi ila unabomoa. Bora nikae tu kimya.

Over Ze Weekend: Una mpenzi?

Muna: Ndiyo…ninaye.

Over Ze Weekend: Unawezaje kuwa na mpenzi wakati mafundisho yanakataza?

Muna: Nilikuwa naye kabla hata sijaokoka. Kwa hiyo sina budi kuendelea naye na kuendelea na taratibu nyingine hata tufikie ndoa.

Over Ze Weekend: Naye ameokoka?

 

Muna: Anamwamini Mungu, lakini taratibu nitamuombea hadi aokoke.

Over Ze Weekend: Lakini inasemekana unatoka kimapenzi na muimba Injili aitwaye Joel Rwanga?

Muna: Hapana. Nipo naye tu karibu na ninashirikiana naye kuandaa tamasha la Injili liitwalo New Beginning au Mwanzo Mpya Tumaini Jipya

 

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.