Mungu aliyekupa, amemchukua na ndiye atakupa mwingine

-81e75695ec0f839dAsante Mungu Valentine’s Day imepita salama hapo jana (Jumapili) japokuwa najua wapo waliopata misukosuko ya hapa na pale. Natumia nafasi hii kuwatakia mfungo mwema (Kwaresma) kwa Wakristo wote duniani na mfungo huu uwe mwanga wa maisha yetu mema kwa siku zote.

Mada ya Jumatatu hii inalenga kuwafariji wale wote ambao wamefikwa na masaibu mbalimbali kwenye uhusiano wao, hasa wale ambao wenza wao wametangulia mbele ya haki (wameaga dunia) mara tu baada ya kuanzisha uhusiano wao. Poleni sana!

Msomaji ambaye pengine unahisi kama ni mtu mwenye mikosi katika uhusiano kwa kupata mchumba, mke au mume na ndani ya muda mfupi akafariki dunia akiwa mikononi mwa penzi lako, tafadhali usiwaze wala kusononeka moyoni, ndivyo dunia ilivyo.

Ni kweli ulimpenda, alikuheshimu na pengine alikuwa msaada na tegemeo katika maisha yako na watu wengine waliowazunguka. Pamoja na hayo yote, nakusihi usisononeke, ulimpenda ila Mungu amempenda zaidi.

Amini nakwambia, Mungu ndiye aliyekupa, ndiye aliyempenda zaidi yako na Mungu huyohuyo atafanya njia pasipo na njia, naamini atakupa mwenza mwingine atakayerejesha furaha ya maisha yako daima.

Najua ni namna gani unaumia, pengine uchumba au penzi lenu lilikuwa bado bichi, bado pevu kama mwezi angavu mara umpendaye akakutoka, inauma, inasikitisha kibinadamu, inakatisha tamaa, wakati mwingine unahisi hautapenda na wala hautapata tena mpenzi mwingine kama yule, la hasha! Utapata, mwamini Mungu hajawahi kushindwa na wala hatashindwa.

Usijione huna thamani ya kuwepo au kuishi katika dunia hii bila ya uliyempenda. Yawezeka ilikuwa ni siku chache tu tangu ajitambulishe au umtambulishe kwa wazazi wako au tangu akuvishe pete ya uchumba na pengine tangu mfunge ndoa au mlipotoka tu kwenye fungate (honeymoon) naye akatoweka duniani.

Ni vigumu kuvumilia kwa mtu uliyempenda, uliyemthamini akakuthamini, mliyependana na kuheshimiana, mliyefurahia penzi lenu, leo haupo naye kimwili, ingawa kiimani unaweza kuendelea kuwa naye.

Safu hii ya XXLove inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki, wapenzi, wachumba au wanandoa waliofiwa na wenza wao, tambua kuwa pamoja na yote hayo, maisha bado yapo na yanatakiwa yasonge kwani sote ni wasafiri.

Na hata dini zetu zinaamini katika uwepo wa kifo kama njia ya kurejea kwake muumba, hivyo jipe moyo, tumaini kuwa ipo siku utapata tena neema.

Kweli kuna pengo kubwa kuanzia moyoni hadi maishani mwako, kuna kitu cha kipekee unakimisi kutoka kwake, unamisi tabasamu, utani, ucheshi nk.

Unakumbuka mengi, rangi za nguo alizokuwa akizipenda, chakula alichokipenda, harufu ya manukato na unakumbuka ustadi wake mlipokuwa faragha.

Mpenzi msomaji pata japo muda mchache wa kumkumbuka ndugu, rafiki, mpenzi, mke au mume wako aliyetangulia mbele za haki, muombee bila kujali alikufa mkiwa katika hali gani, mathalan ya kutoelewana kisha sema Amen!

Tuma maoni yako kama ni mmoja wa walengwa na yatatoka wiki ijayo kwenye safu hii.Kwa habari, ushauri zaidi kuhusu mapenzi, tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Facebook, tu-follow Insta:@mimi_na_uhusiano au kujiunga kwenye group letu la WhatsApp.

Loading...

Toa comment