The House of Favourite Newspapers

Musonda Awapa Mchecheto TP Mazembe Kombe la Shirikisho Afrika

0

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mzambia, Kennedy Musonda, amemaliza majukumu yake ya timu ya taifa, na sasa nguvu na akili zake anazielekeza katika mchezo wa mwisho wa hatua ya ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mchezo huo, Yanga inatarajiwa kuvaana dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Aprili 2 kwenye Uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi huko nchini DR Congo.

Mchezo wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga ilifanikiwa kuwafunga TP Mazembe mabao 3-1 yaliyofungwa na Mudathiri Yahya, Tuisila Kisinda na Musonda mwenyewe.

Akizungumza na Spoti Xtra, Musonda alisema kuwa bado wana uhitaji wa pointi tatu za TP Mazembe zitakazowawezesha kumaliza katika Kundi D wakiwa kileleni.

Musonda alisema anaamini mchezo huo hautakuwa mwepesi kwao, lakini kama wachezaji wanataka kuendelea kuwapa furaha mashabiki wao kwa kupata ushindi ugenini.

Aliongeza kuwa, amepanga kutumia kila nafasi atakayoipata kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga kwa wenzake ili wafanikishe malengo hayo ya kumaliza wakiwa kileleni.

“Nimemaliza majukumu ya timu ya taifa, sasa nguvu na akili zangu sasa unafikilia mchezo wa Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ambao ni muhimu kwetu kupata ushindi katika pambano hilo.

“Ninaamini kwa umoja na ushirikiano uliokuwepo kwetu wachezaji, tutapata ushindi mbele ya wapinzani wetu ambao watakuwa nyumbani wakipata sapoti kubwa ya mashabiki.

“Niwaombe mashabiki wa Yanga waungane na timu katika safari ya kuelekea Congo kwa ajili ya kutusapoti tutakapokuwepo uwanjani tukiipambania timu,” alisema Musonda.

Leave A Reply