The House of Favourite Newspapers

Mussa Sima: Ni Kazi Kubwa, Tumpongeze JPM kwa Kura

0

MGOMBEA Ubunge katika jimbo la Singida Mjini, Mussa Sima (CCM) amewataka Watanzania kumpongeza Mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli kwa kumpatia kura za kutosha ifikapo Oktoba 28 mwaka huu kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kwenye kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

 

Sima ametoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi wa jimbo la Singida mjini na kuwaomba kumpatia kura za kutosha ili aendelee kumsaidia Dk. Magufuli katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini.

Alisema baadhi ya mambo Dk. Magufuli aliyoyafanya katika kipindi chake ni kurudisha nidhamu ya watumishi.

“Ninyi ni mashahidi, miaka mitano nyuma na hii tuliyoingia sisi namna nidhamu ilivyoboreshwa, hivi ni vigezo ambavyo wameviangalia na kuifanya Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kati. Sisi ilikuwa ni kutekeleza tu na tumetekeleza kweli.

 

“Lakini amesimamia matumizi bora ya fedha za umma, katika nchi 186 duniani, Tanzania ni nchi ya 28 kwa matumizi bora ya fedha za umma. Nataka niwaeleze mjue, tuko kwenye mchakato wa uchaguzi lakini kazi mliyotutuma tumeifanya, tunapoomba ridhaa ya pili muwe na uhakika kwamba tutaifanya zaidi ya tulivyofanya mwanzo.

“Kwa sababu inawezekana tuliingia kwenye kipindi kigumu, leo tunaingia tukiwa wazoefu. Kenya ni nchi ya 70 Uganda ni nchi ya 100, kwanini msimpongeze Magufuli.  Mzee wa watu hawezi kutoka jasho kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa Watanzania. Tunatakiwa tutoke jasho sisi kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha anapata kura za kutosha,” alisema.

 

Aidha, alisema katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Dk. Magufuli, amenunua ndege nane mpya.

“Walisema Tanzania hawajanunua ndege lakini ukiwasikia leo wanasema wamenunua ndege hawajawashirikisha watanzania.

“Niwaambie ukweli miaka ya nyuma tulikuwa tunakodisha ndege moja kwa dola za Marekani milioni 43 inafanya kazi miezi tisa tu, miezi mingine 36 ipo gereji. Dk Magufuli amenunua ndege mpya moja kwa Dola milioni 32, tunakodisha kwa milioni 43, mnataka afanye nini.

 

 “Lakini anasimama mtu mwingine anasema wamekosea kununua ndege, hawajashirikisha watanzania, namshauri arudi nyuma asiwahaulishe watanzania, na mimi nimeamua kuwakumbusha ili mjue tulikuwa tunaingia gharama kubwa sana, unakodisha ndege milioni 43 miezi tisa ipo gereji leo tumenunua mpya nane,’ alisema.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply