MUUZA SUPU, MTEJA WAZICHAPA LAIVU

MBEYA: Ni jambo litakaloku-shangaza lakini limetokea hivi karibuni katika jiji la Mbeya ambapo muuza supu mmoja alizichapa kavukavu na mteja wake. 

 Kuzichapa huko kunaharibu ule usemi wa wahenga unaosema ‘Mteja ni Mfalme’ kwani kwa muuza supu huyo, aliuweka kando. Habari zinasema kisa cha vijana hao kuchapana kinachekesha kwa sababu kinatajwa kuwa ni shilingi 500 tu.

 

Vijana hao ambao majina yao hayakutambuliwa mara moja inadaiwa mmoja alikuwa ni mteja na alikunywa supu asubuhi hiyo na ulipofika wakati wa malipo, yeye anadai alilipa shilingi elfu moja kabla. Muuza supu kuambiwa hivyo akaja juu na kudai kuwa hajalipa chochote, hapo ndipo varangati likaumuka. Mteja akidai ametoa shilingi elfu moja na anadai shilingi 500 na muuza supu akisisitiza kwamba hajalipwa hata senti tano na anadai shilingi 500.

“Mabishano hayo yalisababisha wawili hao kushikana mashati, wakaanza kupigana hadharani na kujaza watazamaji,” alisema shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina la John Mwamwaja.

 

Alisema tukio hilo lilivuta watu wengi na kusababisha kujitokeza kwa wasamaria wema ambao waliamua kuwachanisha vijana hao. “Lakini waliumizana kwa sababu waliangushana na wakabingirika hadi kwenye mtaro, kwa kweli ilikuwa kitimtimu eneo hilo,” alisema John.

 

Alipoulizwa sakata hilo liliishaje alisema baada ya kuachanishwa yule mteja aliondoka na kuelekea kusikojulikana, hivyo hakuna aliyepata haki yake waliyopigania. “Muuza supu aliyekuwa anadai shilingi 500, hakuipata na mteja aliyekuwa akidai shilingi 500, naye hakuambulia kitu na ugomvi ukaishia hapo,” alieleza shahidi huyo.

Baadhi ya wasamaria wema walisema ugomvi huo uwe fundisho kwa watu wanaodaiana kwa sababu kungetumika lugha ya maelewano wala wasingefikia hatua ya kupigana ngumi kiasi hicho.

 

“Mara zote kunapotokea mabishano kinachotakiwa kila mmoja kuwa na subira na kumsikiliza mwenzake lakini hawa walikuwa hawasikilizani hata kidogo ndio maana kukatokea varangati lile,” alisema shuhuda mwingine ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu la Issack.
Toa comment