The House of Favourite Newspapers

Muwasho na kutokwa na majimaji ukeni (Vaginal Discharge)-2

0

Diagnose-Vaginal-Discharge-Step-6-Version-4Wiki iliyopita nilianza kuzungumzia aina za magonjwa yanayohusiana na mwanamke kupata muwasho na kutokwa na majimaji ukeni. Wiki hii naendelea…

TRICHOMONIASIS

Ugonjwa wa Trikomonia husababishwa na vimelea viitwavyo ‘Trichomonas Vaginalis’. Huambatana na kutokwa na majimaji mepesi sana ukeni, yapo kama usaha yaani ya njano, yana harufu mbaya ambayo hata mtu wa pembeni huhisi.

JINSI UGONJWA UNAVYOTOKEA

Ugonjwa huu huonyesha dalili za moja kwa moja kwa mgonjwa. Wanawake wengi wenye tatizo la kutokwa na majimaji ukeni na muwasho ndani ya uke huwa na tatizo hili.

Ugonjwa huu kwa asilimia kubwa huenezwa kwa ngono. Mwanaume akiupata hulalamika kuwashwa uume mara baada ya ngono na baada ya muda muwasho hutoweka wenyewe. Hadi ugonjwa kujitokeza tangu ulipofanya ngono ni siku nne hadi 28.

DALILI ZA UGONJWA

Kama tulivyoona hapo mwanzo ni kutokwa na majimaji mepesi ya njano na yenye harufu mbaya ukeni, kuhisi kama joto ukeni, muwasho ukeni kwa ndani na kuwa na hamu au raha ya kujikuna ukeni kwa ndani, maumivu wakati wa kukojoa mkojo au moto kwenye njia ya mkojo, kwenda haja ndogo mara kwa mara, maumivu wakati wa kujamiiana, kutokwa na damu baada ya ngono.

Pamoja na uchafu kuwa na rangi ya njano kiasi, lakini asilimia kubwa ya hayo majimaji huwa ya kijani na harufu mbaya. Mwanamke akichunguzwa ukeni huwa na makovu ya kujikuna au sehemu za ukeni huwa nyeusi sana.

Ugonjwa huu hufanana kwa karibu na ugonjwa wa kusinyaa uke na kuharibika kwa ngozi ya ukeni.

MADHARA

Ugonjwa huu husababisha vidonda vikubwa visivyopona haraka ukeni, kuharibika shingo ya kizazi na hatari ya saratani. Pia mirija ya uzazi inaweza kuziba na kusababisha ugumba.

UGONJWA WA KISONONO

Ugonjwa huu huitwa ‘Gonorrhoea’ au Gono kama wengi walivyozoea kuita. Athari kubwa za ugonjwa huu hujionesha kwenye njia ya mkojo.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Ugonjwa huu husababishwa na bakteria aitwaye ‘Neisseria Gonorrhoea’ kitaalam maarufu kama’Gram-negative Diplococcus’ ambapo hukaa zaidi kwenye njia ya mkojo, mdomo wa kizazi, kwenye njia ya haja kubwa au kinywani.

Bakteria hushambulia kizazi hasa mirija ya uzazi na kusababisha tatizo la mirija liitwalo ‘Salpingitis’. Ugonjwa husambaa kwa ngono na tangu upate maambukizi hadi kujifungua huchukua wastani wa siku tatu hadi tano.

DALILI ZA UGONJWA

Wanawake wenye Gono huwa hawana kabisa dalili katika hatua za awali kwa hiyo mwanaume akifanya naye tu ngono atahisi maumivu na kutokwa na usaha katika njia ya mkojo baada ya siku tatu.

Mwanamke mwenye Gono hupata maumivu chini ya tumbo, sehemu ya nje ya uke huwa nyekundu, huvimba na maumivu makali na usaha. Uke kwa ndani pia huvimba na kuuma na kunakuwa na usaha.

Hali hii huendelea na kuathiri shingo ya uzazi na njia ya mkojo, kuhisi kwenda haja ndogo mara kwa mara lakini unaogopa kukojoa kutokana na maumivu.

Mdomo wa uke unavimba na unapata maumivu makali unapoanza kujamiiana.

Mashavu ya uke moja au yote yanaweza kuvimba na kuwa jipu lenye maumivu makali ukashindwa hata kutembea au kukaa.

Utapata muwasho kwenye haja kubwa na maumivu ambapo utatokwa na majimaji au damu katika tundu la haja kubwa na ukadhani ni bawasili kumbe maambukizi ya Kisonono yamesambaa huko.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply