The House of Favourite Newspapers

MUZIKI KONKI, ELIMU KONKI MASTER!

UKISIKIA neno Konki Konki, Konki Master kwa harakaharaka kwanza utamfikiria mkongwe katika Muziki wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya’.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, Dudu Baya aliyewahi kukimbiza na ngoma kibao ikiwemo Nakupenda Tu na Cheka Kidogo amezua gumzo kila kona baada ya kuja na staili ya kuwataja watu wanaodaiwa kuwa ni wanaume tata (mashoga) kwa kuanza na usemi wa Konki, Konki, Konki Master.

 

Kwa mujibu wake, Dudu Baya anasema; “Konki Konki ni mtu aliyefuzu vikwazo vingi, Konki ni msomi, mwanaharakati naweza nikasema kama vile kwenye movies wakina Arnold Schwarzenegger, Rambo na wengineo. Ukija hapa kwenye muziki wakina Bi Kidude na wakongwe wengineo hao ni Makonki. Sasa Konki hii ni lazima uitamke mara tatu Konki, Konki, Konki Master.”

 

Lakini pia ukiachilia aliyosema rapa huyo, kwenye Muziki wa Bongo Fleva napo kuna makonki yaani wamefuzu kuwa mastaa lakini pia ni makonki kwenye elimu yaani wamepata bahati ya kufika hadi elimu ya juu. Showbiz limekuanikia makonki kwenye Bongo Fleva na pia makonki kwenye elimu;

Nikki wa Pili

Ni rapa anayefanya poa akitokea Arusha ‘A Town’ akiwakilisha Kundi la Weusi lenye vichwa hatari kama vile Bonta Maarifa, G Nako na Joh Makini.

Kwenye muziki ameonesha ukonki wake kwa kusumbua kwenye kila ngoma anayotoa ambapo hadi sasa ni ngoma kibao zipo masikioni mwa mashabiki ambazo ni Sweet Mangi, Safari, Nje ya Box, Baba Swalehe na nyingine kibao.

 

Lakini pia kwenye elimu, Nikki ni konki master kwa wasanii wenzake akiwa ametuliza kichwani Shahada ya Uzamili Katika Sosholojia (Masters In Sociology) aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Hamis Mwinjuma

Kama ilivyo kwa Nikki, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ naye alikuwa akiunda Kundi la East Coast Team ‘ECT’ lililokuwa na vichwa hatari kama AY, Snare, Buff G, Pauline Zongo na King Crazy GK.

 

MwanaFA aliyekuwa akiwakilisha pia Jiji la Tanga, kwenye muziki ameonesha ukonki haswaaa! Ukisikiliza ngoma zake zilizotamba ambazo huwezi kuzichoka masikioni mwako kama vile Alikufa kwa Ngoma, Bado Nipo Nipo, Msiache Kuongea, Yalaiti na nyingine kibao utaelewa namaanisha nini.

Mbali na muziki kuwa konki, kwenye elimu pia ni konki master akiwa kichwani na Shahada ya Uzamili Katika Sayansi ya Biashara (Masters of Science in Finance) aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Coventry huko nchini Uingereza.

Vanessa Mdee

Ukimuita Vee Money utakuwa hujakosea sana kwani ni mulemule. Kama ilivyo kwa makonki wengine kwenye muziki, Vee Money ambaye kipaji chake kilijidhihirisha alipoanza utangazaji akiwa MTV Base akawa konki, akaingia kwenye muziki akawa tena konki na kwenye elimu akawa konki master.

 

Tangu ameingia kwenye Muziki wa Bongo Fleva hajawahi kuyumba. Kolabo zake za kimataifa za fastafasta alizoshirikishwa na nyingine kushirikisha ndizo zimemuweka kwenye listi ya makonki kwenye muziki.

 

Sikiliza ngoma kama Nobody But Me aliomshirikisha rapa kutoka Afrika Kusini ‘Sauz’, K.O pamoja na Kisela akiwa na Mr. P ambaye pia ni pacha wa Kundi la P Square kutoka nchini Nigeria. Vee Money ni konki kwenye elimu akiwa amehifadhi kichwani Degree ya Sheria aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Kenya Methodist.

Maua Sama

Akikusimulia muziki wake ulipoanza kutambulika bila shaka ataliingiza jina la MwanaFA. Ni ukweli usiopingika kuwa MwanaFA ndiye aliyethubutu kumchukua na kummeneji enzi hizo alipokutana naye Moshi alipoenda kwenye shoo.

 

Tangu ameibuka na Ngoma ya So Crazy akawa konki, akaja Mahaba Niue akawa tena konki na sasa Iokote amekuwa konki konki hasa. Si kwenye mabaa, bajaj, bodaboda, kumbi za starehe na sehemu nyingine lazima masikio yako yatapisha na Ngoma ya Iokote, kama haijawa inaisha basi itakuwa inaanza kupigwa. Kumbuka kuwa, kwenye elimu pia, Maua ni konki master naye akiwa na Shahada ya Biashara aliyoipata katika Chuo kikuu cha Ushirika na Biashara, Moshi.

 

Makonki wengine Wapo makonki wengine ambao kwenye muziki wameonesha uwezo na pia kwenye elimu ni makonki master nao ni Mo Music mwenye Shahada ya Uhusiano wa Umma na Masoko (Bachelor of Public Relation and Marketing) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino jijini Mwanza. Juma Abdul ‘Jux’ konki wa R&B akiwa na Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Degree ya Computer Science) aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Guadong nchini China.

 

Nahreel ambaye ni konki wa kutengeneza ‘beats’ akiwa na Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Degree ya Computer Science) kutoka nchini India. Billnass ambaye ana Shahada ya Manunuzi na Ugavi (Bachelor Degree of Procurement and Supply) aliyoipata College of Business Education (CBE) jijini Dar.

Bob Juniour ambaye naye ni prodyuza konki akiwa na Shahada ya Uhandisi wa Mifumo ya Mawasiliano (Bachelor Degree of Telecommunication Engineering) aliyoipata huko nchini Finland, katika Chuo Kikuu cha Helsinki.

Comments are closed.