The House of Favourite Newspapers

MVUVI NUSURA ATOLEWE ROHO NA KIBOKO

KIGOMA: Inatisha! Ndiyo neno unaloweza kusema; ni kufuatia kushambuliwa na kiboko na kunusurika kifo kwa mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Dunia Hamis (26) mkazi wa Kijiji cha Nguruka mkoani Kigoma alipokuwa akifanya shughuli za uvuvi katika Mto Malagarasi kwa kutumia mtumbwi.  

 

Akizungumza na Gazeti la Amani Hamis amesema, tukio hilo la kutisha limetokea Januari 14, mwaka huu, majira ya Saa mbili asubuhi alipokuwa akifanya shughuli zake ghafla mtumbwi wake ulishambuliwa na kiboko, ukazamishwa majini naye akajeruhiwa vibaya mguuni na mnyama huyo kabla ya wasamaria wema kumpa msaada.

 

“Nilikuwa nikivua samaki kama ilivyo kawaida kwenye Mto Malagarasi, nikiwa ndani ya mtumbwi, ghafla niliona mtumbwi wangu unanyanyuliwa juu mimi nikiwa ndani yake, kisha ukazamishwa majini.

Muda huohuo nikahisi maumivu makali katika mguu wangu wa kulia, yule mnyama alikuwa ameng’ang’ania mguu wangu huku akiniburuza ndani ya maji,” alisema Hamis. Aliendelea kusimulia kuwa, baada ya mnyama huyo kumburuza majini, bahati nzuri wasamaria wema waliokuwa karibu na mto huo walipambana na kiboko huyo hadi kufanikiwa kumwokoa akiwa amejeruhiwa vibaya mguuni.

 

“Baada ya kuokolewa nilikimbizwa Hospitali ya Kijiji cha Nguruka, nilipewa huduma ya kwanza na kusafishwa jereha baya mguuni mwangu, nikaongezewa na damu, hata hivyo madaktari wa hospitali ya kijiji wamenipa rufaa ya kwenda Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni kwa matibabu zaidi kwani wamesema jereha hili ni kubwa wao hawana uwezo wa kulitibu.”

 

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema, hana taarifa yoyote, isipokuwa atafuatilia kujua ukweli na undani wake. “Sijapata taarifa ya tukio hilo, ingawa natambua taarifa inaweza kufika mezani kwangu muda wowote, nitakapoipokea tu nitatolea ufafanuzi wa jambo hilo,” alisema kamanda Otieno.

 

Hamis ambaye ni baba wa watoto wawili anaomba wasamaria wema popote walipo waweze kumsaidia gharama za matibabu, kwani uwezo wake kifedha ni mdogo na kwamba akizembea kujitibia mguu wake unaweza kukatwa. Namba za simu kwa ajili ya msaada kwa mgonjwa huyo ni 0625 156 296, jina litatokea Malimu Shabani.

Stori: Ally Katalambula, Amani

Comments are closed.