The House of Favourite Newspapers

Mwaka mpya, tujenge nchi kwa pamoja

0

nyerereIjumaa ijayo Watanzania wote tunaingia Mwaka Mpya wa 2016. Kwangu binafsi mwaka 2015 umekuwa wa bahati mbaya ya kukumbwa na balaa baada ya kampuni yetu kupoteza wafanyakazi wawili, Robert Tillya na Haruni Sanchawa, hakika yalikuwa mapigo mazito lakini hayo yote mimi na wenzangu tunamuachia Mungu.

Ndugu zangu,
Kwangu mwaka 2016 nadhamiria uwe ni wa kusonga mbele kwa kila Mtanzania. Na ningependa sote tuwe na dhamira hiyo ya kusonga mbele kama watu binafsi na kama taifa. Tutangulize zaidi masilahi mapana ya nchi yetu kama anavyotuhimiza Rais John Pombe Magufuli.

Naamini wengi wetu kuna mambo ambayo tumeshindwa kuyafanya mwaka huu 2015 kama tulivyodhamiria lakini hilo lisitukatishe tamaa, tuzidi kupambana na kusonga mbele.

Nitapenda mwaka 2016 wote tujikite kwenye kuhamasisha juhudi za maendeleo kwa Watanzania wote hasa kwa vijana wa vijijini na mijini kwani hakuna siri, vijana wa wana changamoto nyingi sana zinazohitaji kutatuliwa ili wafurahie maisha na kulijenga taifa hili ambalo lilipoteza mwelekeo kwa watu kukosa uzalendo wa kweli.

Uzalendo wa kweli ukiwepo katika mioyo yetu, hakutakuwa na ufisadi, kila Mtanzania akimfikiria mwenzake kuwa anahitaji kupata sehemu ya keki ya taifa, hakutakuwa na rushwa. Upate rushwa ili mgonjwa atibiwe na asipokuwa na fedha za kukupa wewe mtoa huduma basi afe, je huo ni uungwana kweli?

Kila mtu pale alipo afanye kazi akijua kuwa taifa linamhitaji na linamuangalia ili alete tija kwa raia hasa maskini wa nchi. Ubinafsi ukiwekwa kando, nchi itaendelea. Mali za taifa ziwe za taifa kweli na zisiwe kwa ajili ya wachache. Haya ndiyo Rais Magufuli anayoyapigania.

Naamini, tukimuunga mkono rais nchi itakuwa safi kimazingira na kiuchumi. Uzalendo uwe mioyoni mwa kila mchapakazi, iwe kampuni binafsi au ya serikali.

Tusikubali ufisadi katika sehemu zetu za kazi kwani jambo hilo linaleta mfarakano. Kwa nini yule apate kingi na wengine wafe kwa kukosa dawa ya malaria? Je, wasomi wanaohujumu nchi wanataka nani atufanyie kazi wakati wao walisomeshwa na taifa ili watutumikie?

Badala ya kututumikia baadhi yao wanatumia dhamana waliyopewa kutokana na elimu yao bora na kuaminiwa na mamlaka zilizowapa kazi, kuhujumu taifa na kutia mifukoni mwao fedha ambazo zingesaidia wananchi, hasa maskini katika nchi hii.

Lakini wizi wa fedha za umma unarudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa sababu barabara, zahanati, madawati ya shule, ujenzi wa majengo ya serikali, ununuzi wa magari ya kuhudumia wafanyakazi na umma wa Watanzania na kadhalika, serikali inashindwa kuhudumia.

Mwaka 2016 nitapenda watu wote wawe walinzi wa mali za umma na aliyepewa dhamana ya kusimamia afanye hivyo bila kusukumwa.

Pamoja na yote hayo, mwaka 2016 nitajitahidi, kuwa pamoja na Watanzania wenzangu, familia yangu na wananchi katika kujenga nchi yetu. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema mjenga nchi ni mwananchi na mvunja nchi ni mwananchi. Nawatakia nyote HERI YA MWAKA MPYA!
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply