The House of Favourite Newspapers

Mwakinyo Kapigwa… Hakuna Anayesema Kitaalamu

0

GUMZO ambalo limetawala katika mijadala ya michezo kwa wikiendi hii ni kwamba bondia Mtanzania Hassan Mwakinyo alipigwa na Arnel Tinampay kutoka Ufilipino.

Pambano hilo la raundi kumi lisilo na mkanda katika uzito wa Super Walter, majaji walimpa ushindi Mwakinyo kwa 97-93, 98-92 na 96-96, yaani Majority Decision (Majaji wawili kutoa ushindi na mmoja sare).

 

Wengi wanaosema Mwakinyo amepigwa wameshindwa kuweka sababu sahihi za kiufundi zaidi ya hisia, wakiamua kutaka kuonekana ni wakweli kwamba eti Mfilipino ameonewa!

Kawaida katika mambo mengi sana nchini, vitu hufuata mkumbo hasa baada ya jambo kuzungumzwa na mtu aliyekuwa akisubiri lizungumzwe aliliona na akawa hana uhakika.

 

Kitakachozungumza au atakachoanza kukisikia mara tu baada ya kuwa akisubiri, kinakuwa ndiyo uhakika na kuingia kwenye mkumbo wa kukisambaza.

Binafsi nina mambo mawili. Pambano lile kama ni matokeo tofauti, lingeweza kuwa sare. Kama ni lazima mmoja ashinde, basi bila shaka wala hofu, Mwakinyo alistahili kushinda.

 

Hapa tena si suala la uzalendo, tunazungumza utaalamu wa mchezo wa ngumi ambao niwe wazi baada ya mchezo huo wa juzi, nimegundua ni kweli ngumi ni mchezo wa pili kwa kupendwa baada ya soka, lakini bahati mbaya watu wengi hawajui namna unavyohesabiwa kama ilivyo kwa soka bao linaingia, offside filimbi inapulizwa au faulo namna watu wanavyojipanga na kadhalika.

 

MFILIPINO BORA:

Ili kuwa wanamichezo sahihi, lazima kukubali kuwa kweli kabisa Tinampay alikuwa bora kwenye maeneo kadhaa kumzidi Mwakinyo.

Moja katika ushambulizi, aliweza kushambulia mfululizo mwanzo mwisho na hii ilitokana na kuwa na stamina ya juu kabisa kuliko Mwakinyo.

 

Tinampay ambaye ana uwezo wa kikimbia hadi kilomita 40 wakati anapokuwa anashiriki maandalizi na Mani Pacquiao, hakuonekana kuchoka kama Mwakinyo na bila shaka angeweza kuendelea raundi nyingine tatu au nne baada ya mchezo.

 

Hili ni jambo ambalo Mwakinyo anatakiwa kulifanyia kazi. Lakini nakataa katakata kusema Mwakinyo hakuwa na stamina, kama ni hivyo basi asingefika raundi ya sita. Kwa ubora wa stamina ya Tinampay, kiwango cha Pacquiao, halafu kamaliza raundi zote, basi yuko vizuri lakini lazima aboreshe kiwango chake.

 

Kingine ambacho ni bora kwake ni usugu na hili liko wazi, unaona Mwakinyo pamoja na kupiga ngumi nzito za “kuua” lakini alitamani pambano liishe lakini haikuwa hivyo. Anayefanya mazoezi na Pacquiao akipokea rundo la ngumi, lazima awe sugu.

 

UDHAIFU WA TINAMPAY:

Pamoja na stamina ya kutosha na kushambulia sana, Tinampay alikosa mambo mawili makubwa.

Uzito wa ngumi: Hakuwa na ngumi bora na ndiyo maana unaona Mwakinyo kamaliza.

 

Shabaha duni: Unaona hakuwa na shabaha katika mambo mawili, uwezo wa kulenga usoni lakini hata yeye kupiga tumbo zaidi ya ngumi. Mwakinyo alimuachia tumbo muda mwingi kuonyesha yuko fiti, hii ilichangia hata kupunguza kasi yake. Kwenye pointi nyingi alipoteza akipiga tumbo huku yeye akidundwa usoni mara nyingi, tena ngumi nzito.

 

MWAKINYO NA SHABAHA:

Hakuna ubishi, Mwakinyo alikuwa na shabaha, ngumi zake zilitua na zilionyesha wazi kuchukua pointi. Huenda aliwakera watu kumuachia Tinampay muda wa kumpiga tumboni na wakati mwingine kwenye glovu zake. Watu wakaona ni ngumi na kuona kapigwa sana.

 

Vizuri alifanya hivyo kwa kuwa hakuwa na stamina sahihi ya kupambana na Tinampay na angefanya hivyo bila kumuachia apige achoke, basi Mwakinyo angekwama hata katika raundi ya saba tu. Maana yake, kiufundi alikuwa mjanja na aliusoma mchezo baada ya kuanza kuzichapa tu.

 

HESABU YA POINTI:

Ngumi za kulipwa, zinahesabiwa tofauti na zile za ridhaa. Katika hizi za kulipwa kuna mfumo wa “The 10-point Must System”.

Kila bondia anakuwa na pointi 10 raundi inapoanza na majaji wanaanza kuziondoa au kuzibakiza kutokana na matukio.

 

Ndio maana raundi ikiisha jaji anatoa 10-9 au 10-8 na kadhalika, kutokana na raundi ilivyokuwa.

Bondia akiangushwa pointi moja inaenda, akiangushwa tena, moja inaenda au akifanya madhambi akaonywa na kurudia pointi inakwenda.

 

Mara nyingi kama bondia anatawala raundi kwa ngumi nyingi nzuri bila ya kumuangusha mpinzani huwa ni 10-8 ingawa anaweza kupata 10-9 kulingana na jaji alivyoona.

Wenyewe wanasema wanaangalia zaidi “Effective Aggression” namna ya kutawala raundi kwa kupiga ngumi bora, jambo ambalo Mwakinyo alilifanya zaidi ya Tinampay.

 

Pili wanaangalia “Ring Generalship”, namna bondia anavyombana na kumdhibiti mpinzani wake, hapa Tinampay alikuwa bora zaidi. Defence, hapa ni ulinzi. Bado Mwakinyo pamoja na kupoteza stamina, alikuwa bora kwa kuwa alilinda uso sehemu inayozaa pointi na kumuacha Tinampay akipiga tumbo na kiuno kabla ya yeye kumshushia ngumi tofali.

 

Kitu cha mwisho wanachoangalia katika raundi ni “Hard and Clean Punches”, ngumi sahihi kwa ubora na uhakika. Hakuna ubishi, hizi alipiga zaidi Mwakinyo na kama hukuona vizuri, maji kutoka katika nywele za Tinampay yanaweza yakakukumbusha.

 

Hakuna ubishi kuhusu ushindi wa Mwakinyo. Anayeona ameshindwa, bora angelia na sare na si kusema Mwakinyo alipoteza.

Kwa Mwakinyo, kuna mambo mengi ya kujifunza kwa Tinampay, anaweza kuyafanyia kazi na kuachana na hizi kelele za wale wasiojua alichokifanya. Mwisho pongezi na umeliwakilisha taifa vizuri kwa kuwa hukupigwa.

 

Kwa promota Jay Msangi, naye tumshukuru, ameonyesha hakuna longolongo, kamleta Tinampay bondia kutoka kwa Pacquiao na hata tulipokutana nilimueleza hofu yangu kama tumemuwahisha Mwakinyo.

 

Lakini ni jambo jema kwa kuwa litamkuza zaidi Mwakinyo ambaye hakika amebadilika kwa maana ya speed na hatua ulingoni lakini vizuri amtafute Rashid Matumla “Snake Man’ niliona ana ushauri mzuri wakati akichambua katika runinga ya Azam TV.

MAKALA | Makala- Bongo | SALEH ALLY

Leave A Reply