Mwakinyo Kuwania Mikanda Miwili Dhidi ya Muargentina
BONDIA bingwa wa mabara wa uzito wa superwelter, Hassan Mwakinyo, anatarajiwa kuutetea mkanda wake wa Chama cha WBF, Novemba 13 dhidi ya Jose Carlos Paz wa Argentina.
Pambano hilo lililopewa jina la Dar Fight Night limeandaliwia na Kampuni ya Jackson Group Sports.
Mbali ya kutetea mkanda huo, Mwakinyo pia atawania ubingwa wa mabara wa uzito huohuo wa Chama cha IBA, ambapo pambano hilo litafanyika kwenye Ukumbi wa Next Door Arena.Mkurugenzi wa The Jackson Group Sports, Kelvin Twissa, amesema siku hiyo mabondia kutoka nchi tano watazichapa kumsindikiza Mwakinyo.
Twisa alisema aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika kutoka Kenya atazichapa na Patience Mastara wa Zimbabwe, Zulfa Yusuph Macho atacheza na Alice Mbewe wa Zimbabwe.
Aidha, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ atacheza dhidi ya Alex Kabangu wa DR Congo.Alisema kuwa wameamua kuingia kwenye mchezo wa ngumi kutokana na kutambua vipaji vya mabondia mbalimbali hasa Mwakinyo ambaye anafanya vizuri katika mapambano yake.
Alisema kuwa kampuni yao chini ya udhamini wa Azam TV na Asas ina uzoefu mkubwa katika kuandaa matamasha, masoko na shughuli mbalimbali na kuahidi kufanya jambo la kihistoria hapa nchini.Mwakilishi wa WBF nchini Tanzania, Chatta Michael alisema kuwa rais wa shirikisho hilo, Goldberg Howard atasimamia mapambano hayo.