The House of Favourite Newspapers

Mwakyembe Aongoza Mazishi ya Rweyemamu

0
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harisson Mwakyembe (mbele) akitoa heshima kwenye mwili wa Muhingo Rweyemamu leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harisson Mwakyembe leo aliongoza mazishi ya aliyekuwa mwanahabari nguli nchini, Muhingo Rweyemamu ambaye alifariki dunia Jumamosi iliyopita katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar ambapo shughuli ya kuuaga mwili wake ilifanyika katika Kiwanja cha Mnazi Mmoja na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, dini, wanahabari na wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda akitoa heshima zake kwenye mwili wa marehemu.

Wengine waliokuwepo kwenye shughuli hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, wakuu wa wilaya wastaafu, Halima Kihemba, Jaquiline Liana, Manzie Mangachie na viongozi wengine wa chama na serikali.

 

Diwani wa Mwananyamala, Songoro Mnyonge (Mbele) akifuatiwa na Mhariri wa Uwazi, Elvan Stambuli wakienda kuaga mwili leo.

Taasisi mbalimbali viongozi wake walihudhuria shughuli hiyo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo aliongoza baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, viongozi wengine waliohudhuria ni Absolom Kibanda (Habari Corporation), Tido Mhando (Azam), Julius Mapunda (Tazama), Frank Sanga (Mwananchi), Mkurugenzi wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan, mwakilishi mmoja kutoka Baraza la Habari Tanzania, pamoja na wandishi wa habari.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo, akiwapa pole wafiwa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Theophil Makunga alisema marehemu ilikuwa apelekwe India kwa matibabu lakini daktari wake alishauri amwangalie kwa siku mbili ili afya yake iimarike lakini kwa bahati mbaya, Mungu akamchukua.

“Tulichangishana na tulikuwa tupo tayari kumsafirisha kumpeleka India lakini Mungu akampenda zaidi,” alisema Makunga.

 

 

Waziri wa Habari, Dk Harisson Mwakyembe ( wa pili kushoto) akizungumza na wakuu wa wilaya waliohudhuria kwenye shughuli ya kuuaga mwili wa Muhingo Rweyemamu leo.

Baadhi ya wakongwe katika tasnia ya habari walikuwepo ni pamoja na Salva Rweyemamu, Prince Bagenda, Midladjy Maez na Abdallah Majura, ambapo viongozi wote waliopewa nafasi ya kuzungumza walisema Rweyemamu alikuwa kiongozi na mwalimu katika tasnia ya habari nchini na mchochea maendeleo kote alipopita.

 

Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Stambuli (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe leo Mnazi Mmoja wakati wa kuaga mwili wa Muhingo Rweyemamu.

Licha ya kufanya kazi ya habari, mwaka 2012 aliingia serikalini alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, akahamishiwa Makete kisha Morogoro Mjini. Alizikwa katika Makaburi ya Kinondoni.

 

Baadhi ya waombolezaji wakisikiliza hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na viongozi mbalimbali kabla ya kuaga mwili wa Muhingo Rweyemamu leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Mshereheshaji wa shughuli hiyo ambaye pia ni gwiji katika tasnia ya habari, Abubakar Liongo alisema, siku ya leo ambayo Rweyemamu anazikwa ni siku yake ya kuzaliwa.

 

Na Elvan Stambuli.

SHUHUDIA VIDEO YA KUAGA

Leave A Reply