Mwalala: Kwa Farouk, Yanga Imelamba Dume

KOCHA Mkuu wa Bandari ya Kenya, Bernard Mwalala ameweka wazi kuwa kama Yanga itakamilisha usajili wa kipa wake, Farouk Shikalo ‘Wazza’ basi watakuwa wamelamba dume.

 

Mwalala ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga, kwa sasa anainoa Bandari inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya. Akizungumza na Championi Jumamosi moja kwa moja kutoka Mombasa, Kenya, Mwalala alisema kuwa, licha ya kipa huyo kuwa na mkataba mrefu na timu yake lakini hawezi kumzuia iwapo Yanga watampa ofa nzuri.

 

“Kiukweli suala la Shikalo nalijua kwa kuwa nafahamu kuna baadhi ya viongozi wamezungumza na mchezaji ila kwa upande wa uongozi bado haujui kitu kwa sababu mchezaji bado ana mkataba mrefu na sisi.

 

“Hata yeye hajanieleza chochote pengine bado hawajafikia kwao kwa kuwa hata nilivyokuwa nacheza, nilikuwa naongea na timu kabla ya kuwaambia waende kwa uongozi.

 

“Binafsi Shikalo ni kipa mzuri kwa sababu ndiyo nafanya naye kazi na siku zote akikaa golini huwa naona kama wapo wachezaji wawili maana anajua kuzuia goli vizuri, atawasaidia sana Yanga na kuwapa ubingwa.

 

“Akiwa langoni anajua kazi yake vizuri na siwezi kumzuia kwenda Yanga, akinifuata nimpe maelekezo nitamwambia namna ya kuishi Dar es Salaam kwa sababu nimecheza Yanga na naijua vizuri,” alisema Mwalala.

Ibrahim Mussa


Loading...

Toa comment