MWALIMU AMWANDIKIA DENTI BARUA YA MAPENZI, ANASWA!

 HII ni aibu ya mwaka 2019! Wakati jamii ikiamini walimu ndiyo wanaopaswa kuwa mstari wa mbele kuwafundisha maadili wanafunzi wao, mambo yamekuwa tofauti baada ya barua ya kimapenzi ya mwalimu iliyokuwa inakwenda kwa mwanafunzi wake kunaswa na kuanikwa hadharani, Risasi Jumamosi lina habari kamili.

 

Tukio hilo lilitokea hivi karibuni ambapo mwalimu wa kituo cha masomo ya ziada (Tuition) kiitwacho Goshen kilichopo karibu na Kanisa la TAG Madini, Kata ya Iyela jijini Mbeya, Uswege Mwakijoja alidaiwa kumuandikia barua mmoja wa wanafunzi wake (jina tunalihifadhi kwa sababu maalum) ya kumtongoza iliyojaa maneno matamu ya kimahaba.

 

SI MWANAFUNZI MMOJA

Mbali na mwanafunzi huyo, mwalimu huyo amelalamikiwa pia kufanya kitendo hicho kwa wanafunzi wengine waliokuwa wanasoma katika kituo hicho.

“Yaani huyu mwalimu alikuwa ni tatizo kubwa sana hapa mtaani kwetu, alikuwa akiwasumbua sana watoto wetu kwa kuwataka kimapenzi,” alieleza mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Muddi Kiseji.

 

MZAZI AZUNGUMZA

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi waliokumbwa na tatizo la mwalimu huyo, Frola Njumbo, alisema binti yake ambaye anasoma kidato cha kwanza alimletea barua iliyoandikwa na mwalimu Mwakijoja ikionesha kumtaka kimapenzi mwanaye huyo ili amsaidie katika masomo yake.

 

TUISOME KIDOGO BARUA…

Barua hiyo ambayo Risasi Jumamosi linayo nakala yake, ilionesha mwalimu huyo akimuomba binti huyo awe mwenzi wake huku akimpa ahadi kemkemu.

Miongoni mwa ahadi alizomuahidi ni pamoja na kumwambia anatamani kumsapoti ili aweze kusoma mpaka chuo kikuu, pia kumpa zawadi yoyote aipendayo pindi tu atakapomkubalia ombi lake.

“Kwa jinsi ninavyokupenda siwezi kumaliza yote kuelezea ila wewe nipe nafasi utaona vitendo na kukupatia kila huduma ili uzidi kung’ara zaidi ya sasa…” sehemu ya barua hiyo ilisomeka hivyo.

FULL KUMMWAGIA SIFA

Mbali na ahadi, ticha Mwakijoja alimmwagia sifa ‘kedekede’ denti huyo huku akimsihi ampe nafasi katika moyo wake ili waweze kufaidi mema ya nchi.

“Una umbo zuri, una sura nzuri zaidi ya malaika, una rangi ya mvuto kama chotara wa kichina… siku ya kwanza kukuona nilichanganyikiwa mpaka nikashindwa kufanya kazi…” ilisomeka sehemu nyingine ya barua hiyo.

 

KIPANDE KINGINE…

Kwenye barua hiyo kuna mahali ticha huyo alihitaji utulivu wa nafsi kwa kupata muda wa yeye kukaa na mwanafunzi wake na kuoneshana mambo mbalimbali ya kuashiria upendo.

“Natamani tubaki wawili tu kila wakati huku nikikulisha vitu vitamu upendavyo, huku nikikupa kila zawadi uipendayo.”

 

HATUA ZACHUKULIWA

Baada ya kupokea barua hiyo, mama huyo alitoa taarifa kwenye uongozi wa Kata ya Iyela kwa hatua zaidi dhidi ya mwalimu Mwakijoja.

Uongozi wa kata ulitoa taarifa dawati la jinsia kwa ajili ya hatua za kisheria lakini kabla hawajafika ofisi za kata hiyo alipofikishwa, mwalimu alitoroka baada ya kuomba kwenda kujisaidia.

Kaimu Mratibu wa Elimu, Kata ya Iyela, Mwalimu Odilia Mwabulambo amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wa kata hiyo akiwemo Frola wakilalamikia utitiri wa vituo vya masomo ya ziada na baadhi vikilalamikiwa kuwarubuni watoto.

Hata hivyo, mratibu huyo wa elimu alicharuka na kuwataka wamiliki wa vituo kusajili ili viweze kutambuliwa na serikali.

 

MWALIMU MWENZIYE AFUNGUKA

Risasi Jumamosi lilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Mwakijoja, Kaminyonge ambapo alikiri kufanya naye kazi na kulifahamu tukio hilo.

“Nilifundisha naye lakini baada tu ya kufanya tukio hilo la huyo mwanafunzi, alitoweka kusikojulikana na hata simu zake hazipatikani,” alisema Kaminyonge.

 

Hivi karibuni kumekuwemo madai mengi katika kata ya Iyela ya kuwepo kwa matukio ya ubakaji ingawa wananchi wa kata hiyo wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

 

WAZIRI ANASEMAJE?

Risasi Jumamosi lilimtafuta Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ili kuzungumzia suala hilo lakini jitihada ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

LIVE: Bunge la 11, Kikao cha Pili MASWALI na MAJIBU

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Toa comment